Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aongeza muda uchunguzi moto K’koo

F65580b415eafb6b3541cd9ab6d26124.png Majaliwa aongeza muda uchunguzi moto K’koo

Thu, 22 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameongeza siku saba kwa timu aliyoiunda kuchunguza chanzo cha kuungua Soko Kuu la Kariakoo, Dar es Salaam.

Awali, Majaliwa alitoa siku saba kuanzia Julai 11 kazi hiyo iwe imekamilika, lakini sasa inapaswa kumaliza Julai 25.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, wakati akiwa katika ziara ya kikazi nchini Morocco, tume hiyo ilimuomba waongezewe muda.

Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza katika Baraza la Eid el Haj lililofanyika katika Msikiti wa Mtoro, Kariakoo, Dar es Salaam.

Alisema timu hiyo imeomba muda zaidi kutokana na kutaka kupanua uchunguzi wao hadi katika uimara wa jengo la soko hilo.

"Sababu ya kuomba muda zaidi ni kwamba wanataka kufanya hadi uchunguzi wa kihandisi katika jengo lenyewe ili kujua ubora wake kama linafaa kuendelea kutumika ama lijengwe jingine," alisema Majaliwa.

Alisema ujenzi wa soko hilo umehusisha saruji hadi katika mapaa yake, uchunguzi huo utasaidia kujua kama mapaa hayo ni salama kwa wafanyabiashara ama la kwa kuwa kuna watu wanafanya biashara chini ya mabawa ya paa la jengo hilo.

Julai 11, mwaka huu, Majaliwa alisema kamati iliyoundwa itafanya kazi na kamati ya ulinzi na usalama iliyoanza kufanya kazi chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na itajumuisha Ofisi ya Rais-Ikulu, Ofisi ya Rais-Tamisemi na Ofisi ya Waziri Mkuu itakayowakilishwa na Mkurugenzi wa Maafa.

Wengine ni vyombo vya ulinzi na usalama ikiwamo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Zimamoto na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Majaliwa alisema kamati hiyo pia itajumuisha Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Majaliwa alisema pamoja na mambo mengine kamati hiyo ingeainishwa mali zilizopotea au kuungua na kujua tathimini ya jengo hilo.

“Tunataka kujua jengo baada ya moto nini kifanyike, kwa sababu mara nyingi kunapokuwa na moto kuta zinakuwa teketeke jengo hili ni imara na wataalamu watatushauri na serikali haitasita kama watasema tujenge lingine tutajenga kwa ajili ya kurejesha wafanyabiashara,” alisema.

Majaliwa alisema endapo itabainika kuna watu walifanya tukio hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Tunatambua Mheshimiwa Rais alipotembelea hapa aliunda tume ya kufanya mapitio mbalimbali dhidi ya tuhuma mlizosema nyie wenyewe, inawezekana sijui labda tume hiyo ilianza kubaini kitu kama kuna uhusiano na wale waliobainika na tume hatua kali itachukuliwa kwa hiyo taarifa ya ile tume itaingia kwenye hii nyingine,” alisema na kuongeza:

“Kitendo cha kuungua soko la miaka mingi lazima kuwe na uchunguzi wa kina hizo ni hatua ambazo tunachukua muwe watulivu, kwasasa eneo hili sio salama kwenu.”

Rais Samia Suluhu Hassan ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama vichunguze ili kufahamu chanzo cha moto katika soko hilo.

Rais alisema kuteketea kwa soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa kuwa licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki.

Chanzo: www.habarileo.co.tz