WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya takribani Sh bilioni 1.5 yanayodaiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia Machi mwaka huu.
Alichukua hatua hiyo katika Kikao Kazi na Waziri wa Fedha na Mipango, Katibu Mkuu, naibu makatibu wakuu na watendaji waandamizi wa wizara hiyo jijini Dodoma juzi.
Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.
Alisema ikithibitika si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.
Alitaja baadhi ya matumizi mabaya wanayotuhumiwa nayo ni malipo yaliyofanyika Machi 31, mwaka huu kupitia vocha 30 ya Sh milioni 251 yakielezwa kuwa ni malipo maalumu bila kutaja kazi hiyo, ni kazi gani na nani aliifanya.
Alisema waliolipwa fedha hiyo hawajulikani huku akihoji, “Kwa hali ya kawaida, watu wanajilipa posho ya milioni 251 (shilingi) kwa kazi maalumu ambayo ni ipi?”
Alisema wafanyakazi wa wizara hiyo wote ni watumishi wa umma na kazi wanazopewa za kusimamia, kuandaa na kukagua ndani na nje ya wizara ni za kawaida na zinajulikana. “Sasa labda makatibu wakuu mtatusaidia ni kazi gani hiyo maalumu inayowawezesha kulipwa milioni 251 tena kwa siku moja,” alisisitiza.
Alisema siku hiyo ya Machi 31 pia zililipwa Sh milioni 198.8 kwa madai kuwa ni posho ya honoraria. Kwa siku moja jumla zililipwa fedha za posho Sh bilioni 449.8.
Aliendelea kutaja tuhuma kwamba Aprili 8, mwaka huu, watumishi 27 wa wizara hiyo walilipwa Sh milioni 44.5 zikiwa ni posho ya kazi maalumu ya wiki nne. Pia Aprili 13, mwaka huu zililipwa Sh milioni 155.
Aidha, Aprili 30, mwaka huu zililipwa Sh milioni 43.9 kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuhifadhi mazingira na siku hiyo hiyo zililipwa Sh milioni 14.4 kwa ajili ya siku ya wanawake.
Fedha nyingine Sh milioni 43 zililipwa siku hiyo na kufanya jumla ya malipo yaliyolipwa siku hiyo kuwa Sh milioni 101.8.
“Yaani mko ofisini mnaandaa mpango wa kuandaa mazingira mnajilipa milioni 43 lakini siku hiyo ikalipwa milioni 14.4 (Shilingi) kwa ajili ya Siku ya Wanawake. Kwa hiyo ikitokea siku ya vijana, siku ya wanawake, siku ya wazee na huku mnajilipa,” alisema Waziri Mkuu.
Aliongeza, “Tuna sherehe ngapi? Je watumishi wanaokwenda kwenye sherehe zile tukiamua kuwalipa tutajenga zahanati sisi? Tutajenga vituo vya afya? Lakini siku hiyo hiyo Aprili 30, zililipwa shilingi milioni 43 na kufanya jumla ya shilingi milioni 101.8 kwa siku moja tu.”
Alisema Mei Mosi asubuhi mwaka huu, zililipwa Sh milioni 184.1 na mchana zililipwa Sh milioni 264 zikiwa ni malipo ya kazi maalumu. “Sisi tulikuwa Mwanza tunasherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani ninyi hapa ndani mnalipana posho,” alihoji Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa Mei 3, mwaka huu, zililipwa Sh milioni 146.5 kwa watumishi 125 zikiwa ni malipo ya kuandaa Mpango Kazi wa Manunuzi kazi ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Tarehe hiyo hiyo zililipwa Sh milioni 171.2 kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge.
“Yaani nyie mmekaa mmesema mnataka kuandaa mpango wa kazi wa manunuzi mnajilipa milioni 146. Hii ni sehemu ya kazi yenu. Kama siyo kazi yenu nani aliwaletea hizo nyaraka mnazozifanyia kazi? Kwa nini wasingepeleka Tamisemi au Mambo ya Ndani huko, nani alileta hapa. Sasa maswali haya mjiulize wenyewe,” alisema.
Alisema kuna orodha ya watu waliolipwa fedha hizo 125 na majina yao yameandikwa kifupi na hayasomeki. “Kwa nini msiandike jina la mlipwaji, kwa nini msiandike jina la mpokeaji fedha na cheo chake, mliogopa nini?” alihoji.
Alisema pia kwa mujibu wa nyaraka zake, kuna mtu anayejiita AIAG/TA amejilipa maeneo mawili ambayo ni posho ya maandalizi ya kazi na ufuatiliaji wa nyaraka na posho ya viongozi kwa ajili ya kupitia taarifa Sh milioni 155.
“Yaani unandaa mwenyewe unajilipa na unakuja kuipitia taarifa hiyo unajilipa. Haiwezekani! Huu si utaratibu kabisa,” alisisitiza Waziri Mkuu. Alisema pia kuna posho zilizolipwa kwa ajili ya kuchambua miongozo ya kazi.
“Jamani kufanya uchambuzi wa nyaraka unajilipa posho milioni 155 (shilingi). Kazi nyingine kuratibu zoezi la ukaguzi unajilipa na posho, kazi nyingine uandishi wa taarifa za ukaguzi. Hii kazi ya ukaguzi hii imelipa posho kwenye maeneo manne,” alisema.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni kuipitia taarifa hiyo ya ukaguzi, kufuatilia, kuchambua muongozo, uratibu wa zoezi la ukaguzi na uandishi. “Haiwezekani huu utaratibu wa wapi wenzangu wa Wizara ya Fedha?” alisema.
Aliwataka watendaji wa wizara hiyo kujenga uaminifu kwa wanaokusanya mapato kwa kufanya kazi kwa uaminifu na alihadharisha kuwa watakaoendelea kucheza na fedha za umma hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Aidha, Waziri Mkuu aliwapongeza watendaji wengine wa wizara hiyo ambao wameendelea kufanya kazi kwa weledi. “Na nimesema hapa si wote wenzenu wachache wanatumia vibaya nafasi zao kutuchafua Wizara ya Fedha,” alisema.