Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa amuagiza Dk Ndugulile kufuatilia harufu ya ufisadi Songea

34989 Pm+pic X-ray

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Songea. Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa amenusa harufu ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma kwa Sh129 milioni.

Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Faustine Ndugulile kubaki mkoani humo na kufuatilia suala hilo ili kumbaini mtu ambaye amehusika katika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo na kisha kumpelekea taarifa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumamosi Januari 5, 2019 wakati alipokua akihutubia wananchi kwenye uzinduzi wa mashine tano za kisasa za X-Ray katika viwanja vya hospitali hiyo.

Amesema haiingii akilini ukarabati utumie pesa nyingi hivyo na amehoji kwa nini  wamemtumia mkandarasi toka Mbeya wakati Songea wapo na kiasi cha fedha kilichotumika cha Sh129 milioni hazilingani na thamani ya ukarabati uliofanywa.

"Nakuagiza waziri (Dk Ndugulile) ubaki Songea kwa ajili ya kufuatilia mchakato mzima wa zabuni na kujua nani aliyehusika kupitisha mchakato huo,” amesema.

“Pia ili tuweze kuchukua hatua na hiyo tume wanayosema wameiunda nimeikataa nataka taarifa kamili," ameongeza.

Amesema Serikali ilipoingia madarakani ilirudisha maadili ya utumishi ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya ili watumishi wawajali wanaowahudumia si kupiga madili.

Majaliwa ametaja mikoa ambayo imeanza kufungwa mashine za kisasa za X-Ray kuwa ni Katavi, Njombe, Nzega- Tabora, Simiyu, Ruvuma na Chato- Geita.

Amesema Serikali itanunua X-ray nyingine 24 za kisasa na kuzifunga katika mikoa iliyobakia ili kupunguza msongamano wa wagonjwa.

Majaliwa amewataka madaktari wasikubali kuchafuliwa, kujengewa chuki na Serikali yao wawaseme ambao wanawaangusha.

Majaliwa amesema hiyo ni heshima ya juu kuzindua mashine za kisasa za X-Ray katika Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake, Dk Ndugulile amesema mashine za kisasa za kidigitali 11 zimenuniliwa kwa Sh2 bilioni na zinafungwa katika hospitali za Chato, Katavi, Ruvuma na ndani ya dakika tano unapata majibu dakika 10 zinafika Dar es Salaam na kusomwa na daktari bingwa na kurudishiwa majibu.

Ameagiza ujenzi wa hospitali za wilaya ya Namtumbo, Nyasa, Songea uanze mara moja na ukamilike Juni mwaka 2019 kwani fedha hizo zipo kwenye akaunti za halmashauri zao.

Naye mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameishukuru Serikali kwa kuweza kufunga mashine hiyo ambayo alisema itaondoa adha ya wananchi kukaa foleni muda mrefu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Songea Mjini (CCM) Dk Damas Ndumbalo ameomba Serikali ijenge kituo cha damu salama katika Mkoa wa Ruvuma ili iweze kuondokana na adha ya kutegemea damu salama toka jijini Mbeya.



Chanzo: mwananchi.co.tz