Singida. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi kwa kuamua kuchapa kazi na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
“Moja ya Halmashauri zilizotulia ni Ikungi. Hii ni Halmashauri pekee ambayo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wake wanaongea lugha moja. “Endelezeni kazi hii nzuri ili viongozi wengine waje kujifunza kwenu,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa watumishi waliohudhuria mkutano wa hadhara.
Majaliwa alitoa pongezi hizo jana jioni Ijumaa, Oktoba 4, 2019, wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa halmashauri hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Ikungi.
Aliwataka watumishi wa Halmashauri hiyo watambue wako chini ya wananchi na kwamba bila ya uwepo wao, hata wao wasingepata kazi wilayani humo.
“Mimi na ninyi sote ni watumishi wa hawa wananchi. Bila wao, tusingekuwa na utumishi hapa. Lazima mtambue kwamba mmeletwa hapa ili muwahudumie wao,” alisisitiza.
“Nendeni vijijini, wahudumieni bila kujali umri wao, dini, rangi au itikadi zao. Wakiuliza masuala ya kilimo au maji au afya, washughulikieni na muwape majibu huko huko. Wananchi wengine wanaishi vijiji vya mbali na hapa, wengine hawana nauli, wengine hawajui hata wakija mjini waanzie wapi,” alisisitiza.
Habari zinazohusiana na hii
“Nimekuwa nikisisitiza kwamba wakuu wa idara wasikae ofisini kwa wiki nzima. Nendeni vijijini mkawasikilize wananchi. Wakuu wa idara tofauti, jipangeni mtumie gari moja; siku nne kati ya tano za wiki, nendeni vijijini mkasikilize wananchi na siku mbili zilizobakia mje muandike taarifa zenu ofisini,” alisema.“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi simamieni hili, kwa sababu ni mojawapo ya matakwa ya Serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
Mapema, akitoa salamu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mpogolo alimweleza Waziri Mkuu kwamba uuzaji wa pamba katika wilaya hiyo unaendelea na hadi sasa wameshauza tani milioni 1.4 kati ya tani milioni 2.5 walizojiwekea malengo.
“Pamba imeendelea kununuliwa kwa bei ya Sh1,200 kama ilivyoelekezwa na hadi sasa tani milioni 1.4 zenye thamani ya Sh1.7 bilioni zimenunuliwa viwandani. Tunaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kuwawezesha wananchi hawa kupata fedha hiyo,” alisema.
Alisema anaishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya, mikopo kwa wanawake na vijana, umeme na elimu ambapo ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 64 hadi asilimia 83.
Pia, Majaliwa amemtaka mkuu huyo wa wilaya na mkurugenzi wake wafanye misako kwenye stendi za mabasi ili kuwabaini watoto wasiokwenda shule.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imeondoa michango kwenye sekta ya elimu na kwa maana hiyo watoto wenye umri wa kwenda shule wanapaswa wawe shuleni.
"Michango ya hovyohovyo haipo. Vinginevyo, fedha ambazo wazazi mmeokoa, peleka kwa mtoto. Mnunulie sare, kiatu kizuri, begi la shule na madaftari. Ale vizuri asubuhi na aende shule," alisisitiza Waziri Mkuu.
"Hatutarajii kuona vijana wadogo wanauza biashara kwenye vituo vya mabasi. Mkurugenzi chukua OCD siku moja, nenda kwenye miji yenu midogo, saka watoto wote wanaofanya biashara stendi."
"Watambue wazazi wao, halafu kamata wazazi hao wajieleze ni kwa nini wanawaacha watoto wao waende kuhangaika stendi badala ya kwenda shule. Tunataka kila mtoto wa Kitanzania aende shule," alisisitiza
Alisema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila kijiji kinapaswa kiwe na shule ya msingi na kila shule lazima iwe na darasa la awali ili watoto wenye umri wa miaka minne hadi mitano waanze shule mara moja.