Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na mawaziri na makatibu wakuu kwenye eneo la tenki la maji la kutolea huduma katika ujenzi wa mji mkuu wa Serikali Ihumwa jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, Waziri Mkuu amewaagiza mawaziri wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara na pale watakapojiridhisha kuwa uwezo wao ni mdogo wawabadilishe mara moja.
Ametoa agizo hilo leo akiwa kwenye kikao cha kazi na mawaziri 15 na manaibu mawaziri katika eneo la Ihumwa lililoko kilomita 17 kutoka jijini Dodoma.
“Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati,” amesema.
Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwapa mrejesho mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo jana alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara. “Nataka mawaziri ambao ofisi zao zinajengwa na watu wa Mzinga wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi mkabidhi kwa mkandarasi mwingine,” amesema.
Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wahakikishe wanaongeza idadi ya vibarua ili kazi hiyo iweze kwenda haraka. “Wizara iliyofanya vizuri kuliko zote ni ya Utumishi, wao wako hatua nzuri. Kwa maana ya uchapaji kazi, eneo nililokuta lina wafanyakazi wengi ni Magereza,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimweleza Waziri Mkuu kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.
“Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake,” amesema.
Naye Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amemweleza Waziri Mkuu wizara yake imetoa transfoma tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne ambazo zimejitokeza na kulipia line za transfoma hizo.
“Wizara yetu tumetoa transfoma tisa za kusaidia umeme upatikane eneo la ujenzi. Niwaombe mawaziri waliopo walipie service line tu ambazo gharama yake ni Sh 921,000 ili wafungiwe transfoma na kazi iweze kufanyika mchana na usiku. Hadi sasa, tumeshapokea maombi kutoka wizara nne tu za Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati ili kazi imalizike ndani ya muda mfupi,” alisema.