Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa akunwa mchango wa Asas maendeleo Iringa

710ba58bf1ab62ad8fa854779ca9ddde.png Majaliwa akunwa mchango wa Asas maendeleo Iringa

Wed, 27 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa pongezi na shukrani kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas aliyejenga kiwanda cha ushonaji na ukumbi wa mikutano kwa ajili ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani Iringa.

Miradi hiyo miwili yenye thamani kubwa (haikuwekwa wazi) imejengwa nje kidogo ya mji wa Iringa katika Chuo cha Mafunzo cha Ihemi kinachoendeshwa na UVCCM.

Mradi wa kiwanda una mashine za kushona zaidi ya 100 zinazotumika kuzalisha bendera za chama kwa matumizi ya nchi nzima, sare za wanafunzi na aina mbalimbali za mavazi na mradi wa ukumbi una uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 1,000 kwa wakati mmoja wakiwa wameketi.

Akitoa pongezi kwa niaba ya CCM, Waziri Mkuu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema Asas ni mdau wa kweli wa maendeleo ya chama hicho, mkoa na taifa kwa ujumla na kwamba CCM inamtambua na kuthamini mchango wake.

"Nimefanya ziara mkoani Iringa kama mara tatu au nne hivi, kwa mara ya kwanza nikiwa Naibu Waziri wa Tamisemi. Mara zote ninaposikia mchango wa wadau katika maendeleo ya mkoa wa Iringa lazima jina la Asas litatajwa," alisema.

Alisema mbali na kukichangia chama chake, Asas amekuwa akitoa michango inayofanikisha au kutatua changamoto mbalimbali katika sekta tofauti za maendeleo ikiwamo afya, elimu, michezo na vikundi vya watu na mtu mmoja mmoja.

“Imekuwa vigumu kuyazungumzia maendeleo ya mkoa wa Iringa bila kulitaja jina la Asas hivyo anahitaji kuungwa mkono na kupewa pongezi kubwa,” alisema.

Akikagua maendeleo ya chuo hicho, Majaliwa alisema ni muhimu kwani kinawezesha wananchi kupata mafunzo na ujuzi katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, ufugaji, ushonaji, useremala na ufugaji wa nyuki.

"Wekeni ratiba inayotambulika ili vijana nchi nzima waweze kuja hapa na kunufaika na mafunzo na ujuzi unaopatikana ili wabadili mitazamo kutoka katika dhana ya kuajiriwa kwenda katika kujiajiri," alisema.

Awali, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Raymond Mwangwala alisema Chuo cha UVCCM Ihemi kilianzishwa mwaka 1985 kabla shughuli zake hazijasimama mwaka 1999 na kufufuliwa tena mwaka 2018.

Alisema chuo hicho kinachoendelea kuboreshwa siku hadi siku kinatarajiwa kuwa na aina 21 za mafunzo ikiwamo ushonaji, ufugaji, kilimo na userelema ambayo inatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa vijana na moja ya vyanzo vikubwa vya mapato vya umoja huo.

Alisema katika kukiboresha zaidi chuo hicho, Asas ameahidi kutoa msaada wa mashine za kisasa za useremala ili kuharakisha utoaji wa mafunzo ya kozi hiyo chuoni hapo.

Chanzo: habarileo.co.tz