WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezitaka halmashauri kuwa na mpango wa muda mrefu na endelevu wa kujenga madarasa na vyoo, kutengeneza madawati na miundombinu, badala ya kufanya kwa zimamoto.
Majaliwa alizitaka halmashauri hizo, kujipanga kwa mipango hiyo badala ya kusubiri maagizo ya viongozi wa nchi.
Alitoa agizo hilo jana bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
Majaliwa alisema halmashauri zinatakiwa kuwa na mipango ya muda mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya shule na ziache kufanya kazi hiyo kwa zimamoto, kwani hakuna dharura kwa kuwa kuna takwimu za watoto wanaohitimu shule za msingi.
"Halmashauri nchini zinatakiwa kuwa na mipango ya kudumu ya ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kuingia sekondari kwani takwimu za wahitimu hao zinajulikana," alisema.
Majaliwa alisema halmashauri zinatakiwa kujiandaa, badala ya kungoja viongozi mbalimbali mfano Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu watoe maagizo na matamko ya mara kwa mara.
Alisema wameziagiza halmashauri hizo, kuandaa mipango ya muda mrefu na ya kudumu ili kuchana na mtindo wa zimamoto, kwani zinajua idadi ya wanafunzi wanaohitimu shule za msingi na hata kidato cha nne.
Waziri Mkuu alitoa msisitizo wa msimamo huo wa serikali wakati akijibu swali la Mbunge wa Sengerema, Khamis Hussein Tabasamu (CCM) aliyetaka serikali itoe tamko kwa ajili ya kuchangia fedha kukamilisha maboma ya shule ili kutekeleza agizo lake la kutaka wanafunzi wote waliofaulu ifikapo Febrauri 28, mwaka huu waanze masomo.