Nyang'hwale. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekataa kukagua mradi wa maji wa Nyamtukuza uliopo wilayani Nyang'hwale mkoani Geita kutokana na kujengwa muda mrefu bila kukamilika huku ukiwa na tuhuma za rushwa.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Nyamtukuza leo Jumatano Novemba 28, 2018 katika eneo la mradi huo amesema hana sababu ya kukagua mradi huo ambao hauna maji.
Mradi huo unaojengwa kwa gharama ya Sh15bilioni ulianza mwaka 2014 na ulipaswa kukamilika mwanzoni mwa 2015 lakini hadi sasa haujakamilika.
Kutokana na mradi huo kusuasua Majaliwa ameuhamisha kutoka halmashauri na kutaka usimamiwe na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuanzia sasa na ukamilike kabla ya Juni, 2019.
Waziri Mkuu amekerwa na ufujaji wa fedha za miradi unaofanywa na watumishi wa halmashauri ya Nyang'hwale.
"Hatuwezi kuwalea watumishi wezi wasio waadilifu nataka nikutanishwe nao leo waniambie kwa nini fedha za miradi zikija wanakula," amesema Majaliwa.
Amesema lengo la Serikali ni kumtua ndoo mama kichwani na kusema haitawafumbia macho watumishi wanaofuja fedha za miradi.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema wilaya ya Nyang'hwale imekua kichaka cha wizi, na kwamba tayari miradi yote yenye dalili za ubadhilifu inachunguzwa na Takukuru.
Gabriel alisema mradi wa maji Nyamtukuza ulianza kwa ufisadi na taratibu zote za ununuzi zilikiukwa.
Mbunge wa Nyang’hwale, Nassoro Kasu ameiomba Serikali kuwachukulia hatua watumishi wote waliojihusisha na ubadhilifu wa fedha za miradi, kwamba katika wilaya hiyo Sh3bilioni zilifujwa.