Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ajivunia masoko 28 ya madini

F08ab0c2329a75658fbf2575825ac9b4 Majaliwa ajivunia masoko 28 ya madini

Mon, 21 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema serikali ya chama hicho imeanzisha masoko 28 ya madini likiwemo la Nyamongo, ili kuwainua wachimbaji wadogo ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2015-2020.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini wilayani Tarime, mkoani Mara.

Aliyasema hayo wakati akimuombea kura Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli, wagombea ubunge Michael Kembaki wa Tarime Mjini na Mwita Waitara wa Tarime Vijijini pamoja na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Tarime.

"Kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali za madiniserikali imeanzisha masoko 28 ya madini, vituo vidogo 28 vya ununuzi wa madini na ujenzi wa vituo saba vya mafunzo ya umahiri kwa wachimbaji wadogo vya Bariadi, Musoma, Bukoba, Mpanda, Chunya, Songea na Handeni," alisema Majaliwa.

Alisema uamuzi umesaidia kuongezeka mapato ya serikali, kupata takwimu sahihi za mauzo ya madini, wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika, kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini na kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini.

Pia Majaliwa alisema kwenye biashara ya madini, kodi zenye kero kwa wachimbaji wadogo ikiwemo kodi ya zuio asilimia tano na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18, zimeondolewa.

Akielezea tathmini ya fidia kwa wananchi wa Nyamongo, alisema uthamini kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la maji machafu eneo la Nyamongo kwa vijiji vya Matongo, Nyabichune na Komarera, ulianza Julai, 2019 na malipo ya fidia yalianza kutolewa Mei mwaka huu.

"Hadi sasa shilingi bilioni 32.9 zimelipwa kwa wananchi 1,620 na wananchi 13 wamebaki ambao hawajachukua malipo yao yenye thamani ya shilingi milioni 833. Hao 13 wanasubiri kulipwa kwa sababu walisema hawaridhiki na uthamini wa mali zao, kwa hiyo tathmini itafanyika upya na watalipwa fedha zao," alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz