SERIKALI imeridhishwa na mafanikio yanayotokana na sekta ya madini, ambayo inaongoza kwa kukua kwa asilimia 17 kwa miaka mitatu mfululizo. Pia mapato ya sekta hiyo, yameongezeka kutoka Sh bilioni 168 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 520 mwaka huu wa fedha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alibainisha hayo alipowakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki wakati akifunga Maonesho ya Tatu ya Kimataifa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye sekta ya madini mkoani Geita, yaliyoanza Agosti 17 mwaka huu, Majaliwa aliyataja mafanikio mengine yaliyopatikana katika sekta hiyo kuwa ni udhibiti na usimamizi wa sekta hiyo, kuchochea mwamko wa wananchi kushiriki katika sekta hiyo, wakiwemo wachimbaji na wafanyabiashara ya madini.
Mafanikio mengine ni kuimarisha mifumo ya kisera na kisheria ili taifa linufaike na madini yakiwemo marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017, kuhakikisha madini yanaongezwa thamani hapa nchini, kutolewa kwa leseni zaidi ya nne kwa ajili ya kujenga viwanda vya kusafisha madini ikiwemo dhahabu.
“Mchango wa sekta ya madini ni mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mapato kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 528 mwaka huu wa fedha, lakini pia katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti mapato yaliyopatikana kutokana na sekta hii ni shilingi bilioni 112 na malengo ya baadaye makusanyo hayo yaongezeke hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 600,”alisema Kairuki kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Kutokana na mafanikio hayo, Kairuki aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara ya madini, kuuza madini yao katika masoko ya madini likiwemo Soko Kuu la Dhahabu Geita. Alisema katika nchi nzima, kuna masoko ya madini zaidi ya 31 na vituo vya kuuzia madini zaidi ya 38.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imefuta baadhi ya kodi na tozo kwa wachimbaji wadogo, ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi ya zuio.
Alisema awali kodi yote aliyotakiwa kulipa mchimbaji mdogo ilifikia asilimia 23, lakini Serikali ya Awamu ya Tano imezipunguza na kufikia asilimia 7.3.
“Pia maeneo zaidi ya 23 yameainishwa na kugawiwa wachimbaji wadogo nchini pamoja na leseni zaidi ya 801 za uchimbaji zimetolewa kwa wachimbaji wadogo, lakini pia kutokana na Itifaki ya Nchi za Maziwa Makuu wachimbaji wetu wanaweza kuuza popote duniani madini ya bati baada ya kupewa cheti cha uhalisia cha madini haya,”alisema Kairuki.
Alisema katika miaka mitano ijayo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Awamu ya Tano, itaboresha mazingira yao ya uchimbaji ikiwemo kuwatengea maeneo yaliyofanyiwa utafiti, badala ya kuchimba kwa kubahatisha na kupewa mafunzo ili kuongeza tija ya kazi zao.
Mambo mengine ambayo serikali imeahidi kuyafanya katika miaka mitano ijayo ni kuhakikisha wananchi wanoishi karibu na maeneo ya migodi, wananufaika na madini hayo kupitia mchango wa mgodi kwa jamii (CSR) pamoja na wananchi kupata fursa ya kufanya biashara na migodi mikubwa.
“Naupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa kufanikisha maonesho haya, ni maonesho bora na yanazidi kuimarika kila mwaka. Wito wangu kwa wachimbaji wadogo ni kwamba tumieni ujuzi mlioupata katika maonesho haya kuongeza uzalishaji na mapato kwa kutumia teknolojia bora, pia wamiliki wa leseni kubwa za uchimbaji zingatieni kuwatumia wafanyabiashara wazawa kutoa huduma mbalimbali kwenye migodi yenu,”alisisitiza Waziri Kairuki.
Katika ufungaji huo, Waziri wa Madini, Doto Biteko, aliwataka wawekezaji katika sekta ya madini, kuzingatia sheria na miongozo ya nchi. Alisema serikali imetoa leseni nne kwa ajili ya viwanda vya kusafisha madini katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Geita.
Biteko alisema kutokana na serikali kuboresha sekta ya madini, hivi sasa wafanyabiashara wa Tanzania wanaoongoza kwa kuuza madini ya dhahabu nchini Dubai, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo raia wa kigeni walitawala biashara hiyo.
Kuhusu kuwepo kwa tozo zisizo rafiki kwa wachimbaji wadogo, alisema suala hilo linazungumzika, ila tatizo lililopo ni kwamba baadhi ya wachimbaji wadogo si waamifu, kwa kuwa hawaonekani kwenye mnyororo wa thamani kutokana na kufanya biashara hiyo kwa ujanja ujanja.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, alisema maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa, ikiwemo wachimbaji wadogo kunufaika na mikopo ya mabenki yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni 60.
Alisema katika Mkoa wa Geita kuna masoko tisa ya madini, ambayo yameleta tija katika biashara ya madini. Gabriel alisema mwaka 2016 dhahabu yote iliyouzwa mkoani humo ilikuwa kilo 337.4 yenye thamani ya Sh bilioni 28, lakini kwa sasa dhahabu yote iliyouzwa katika mkoa wake ni kilo 5,591.6 yenye thamani ya Sh bilioni 576.5.
“Mafanikio haya na mageuzi makubwa yanayofanyika nchini, yametokana na mchango mkubwa wa Rais John Magufuli ambaye ni shujaa na mtetezi wa wanyonge, tuendelee kuwaelimisha wananchi kuchagua viongozi bora, kwa kuwa uongozi siyo mashindano ya urembo, tunahitaji viongozi wengi walio kama Magufuli,”alisema.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo za kufungwa kwa maonesho ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, wakuu wa mikoa ya Tabora na Mara na viongozi wa CCM na Serikali. Maonesho ya mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu isemayo “Madini ni Uchumi, 2020 Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Taifa.”