Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aiagiza Tanesco mradi umeme Nyerere

Majaliwa.webp Majaliwa aiagiza Tanesco mradi umeme Nyerere

Fri, 15 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115 na amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, ausimamie ili ukamilike kwa wakati.

Vilevile, Waziri Mkuu amemwagiza mkandarasi anayejenga mradi huo aukamilishe kwa wakati kwa sababu imebainika kuwa mvua zinazoendelea kunyesha nchini haziathiri utekelezaji wa ujenzi huo.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana akiwa katika ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo. Alisema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.

“Nimetembelea eneo la mradi na kujionea shughuli zote zinazoendelea, kazi inayofanyika ni ya uhakika, huku kukiwa na matumaini makubwa ya kukamilisha mradi mapema kabla ya muda uliopangwa.”

Mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji unajengwa na kampuni ya Arab Construction kwa pamoja na kampuni ya Elsewedy Electric zote za kutoka nchini Misri. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha Megawati 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye grid ya Taifa na kuifanya nchi kuwa na umeme mwingi na wa uhakika.

Mbali na kuliwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika, pia mradi huo umewezesha kupungua kwa changamoto ya ajira baada ya Watanzania wengi wakiwamo makandarasi kupata ajira za kudumu na za muda mfupi.

Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitakachosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live