Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa moja ya sifa ya Rais Magufuli ni kusema ukweli na kuutekeleza, hii ni baada ya Rais Magufuli kumpigia simu na kuagiza kuwa ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga unaanza mara moja.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makubaliano ya ujenzi wa barabara ya Ruangwa hadi Nanganga, yenye urefu wa Km 53.2 kwa kiwango cha lami, ikiwa ni ahadi aliyoitoa Rais Magufuli alipofanya ziara Ruangwa.
"Kile ambacho tulikuwa tunatamani, kikaahidiwa hapa na kiongozi wa nchi Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli alipofanya ziara Ruangwa, aliweza kuvunja kiu yetu Wana-Ruangwa toka alivyokuwa anaingia Nanganga wananchi walimuomba asimame na yeye alisimama akijua kuwa, hawa wana hamu ya maendeleo, sifa moja ya Rais Magufuli ni kusema na kutenda na ametekeleza" amesema Waziri Mkuu.
Aidha kwa upande wake Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kwa uhodari wake wa kazi. "Endeleeni kumuani Mheshimiwa Majaliwa, amekuwa akinisaidia, aendelee kuchapa kazi kwa ajili ya Ruangwa na Tanzania".