Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aeleza miaka mitano ya JPM Arusha

6b277f5d35bbffaac9d7f31800a7fad0 Majaliwa aeleza miaka mitano ya JPM Arusha

Mon, 7 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imetoa Sh bilioni 577.53 kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara na kunufaisha wananchi jijini Arusha.

Alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Relini, jijini Arusha, ambapo pia alimuombea kura mgombea urais kupitia CCM, Rais Magufuli, mgombea ubunge Jimbo la Arusha, Mrisho Gambo na wagombea udiwani.

Alisema, kati ya fedha hizo Sh bilioni 1.3 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Arusha na kwamba jengo la wagonjwa wa nje (OPD) limekamilika na ujenzi wa jengo la akina mama ujenzi wake unaendelea.

"Jumla ya Sh bilioni 1.5 zimetolewa kwa jiji la Arusha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya vya Muriet, Kaloleni na Moshono ambapo ujenzi wake umekamilika na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma," alisema.

Majaliwa alisema mbali na ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, pia serikali imetoa Sh bilioni 3.8 kwa ajili ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016–2019/2020 katika jiji la Arusha na upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 98.

Alisema serikali pia imetoa Sh bilioni 2.14 kwa ajili ya kugharamia shughuli za ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu katika shule za msingi 48 jijini humo.

"Sh bilioni 4.68 zimetolewa katika shule za sekondari 29 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule," alisema.

Majaliwa alisema Sh bilioni 1.03 zimetolewa na serikali kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa na vyoo kwa shule za msingi jijini humo, ikiwsmo Olasiti, Daraja II, Oloirien na Sokoni I.

Kuhusu shule za sekondari, Majaliwa alisema serikali imetoa Sh bilioni 4.68 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, mabweni, vyoo na majengo ya utawala, ikiwamo shule za Suye, Muriet, Lemara, Sorenyi, Arusha na Korona.

"Jiji la Arusha linakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo serikali imetoa jumla ya Sh bilioni 520 kwa ajili ya mradi wa majisafi jiji la Arusha ambao utahudumia jiji lote. Utekelezaji wake umefikia asilimia 52," alisema.

Aidha, alisema Sh bilioni 38.4 zimetolewa kupitia Tarura katika kipindi cha 2015/2016 – 2019/2020 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja katika jiji la Arusha, ukiwamo ujenzi wa barabara ya Oljoro – Muriet yenye urefu wa kilomita 2.8.

Barabara nyingine ni za Kisongo Bypass kilomita 3.4, Sokoine –Muriet Meidimu kilomita 8.5, Njiro kilomita 2.8, Ngarenaro kilomita 4.1 na Sombetini kilomita 2.0.

"Barabara ya Arusha –Holili/Taveta ujenzi wa sehemu ya kutoka Sakina hadi Tengeru, kilomita 4.1 na ujenzi wa barabara ya mchepuko ya Kusini (Southern-bypass) kilomita 42.41, ambazo zinajengwa na Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) zitahudumia jiji lote la Arusha na Halmashauri za Wilaya Arusha na Meru," alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Arusha kumchagua Rais Magufuli awe Rais kwa awamu ya pili, kwa kuwa ana uwezo mkubwa wa kusimamia mambo yanayowagusa wananchi na ametekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015 kwa vitendo na sasa anakuja na Ilani mpya iliyosheheni mambo mengi mazuri.

Alisema katika miaka mitano Watanzania wakiwamo wakazi wa Arusha wamenufaika kutokana na miradi ya kimkakati ukiwamo ufufuaji wa usafiri wa treni ya Dar es Salaam hadi Arusha uliokuwa umesimama kwa takribani miaka 30.

Chanzo: habarileo.co.tz