Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa achukizwa DC na DED kutoelewana, atoa maagizo kwa CAG,TBA

75928 Pic+majaliwa

Mon, 16 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amechukizwa na mgongano uliopo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi (DC), Majura Kasika na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo (DED), Mussa Mnyeti, hivyo kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza weledi wa utendaji kazi  wao.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Septemba 16, 2019 na Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Malinyi pamoja na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Toboa, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

“Ni aibu Mheshimiwa Rais John Magufuli amewateua vijana wawe viongozi lakini leo hadi wananchi wa kawaida wanajua mgongano wenu maofisini. Ni aibu Mkuu wa Wilaya ya Mkurugenzi mnagombana tena wakati mwingine mnagombania miradi, mmesahau kutekeleza majukumu yenu,” amesema Majaliwa

Amesema Serikali imewapa nafasi hiyo ili wakasimamie maendeleo ya wananchi na inapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya jamii kama kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara lakini wao wanagombania miradi na mingine wanaichakachua.

Waziri Mkuu amesema mbali na CAG na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwenda kuchunguza utendaji wa viongozi hao, pia ameuelekeza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakakague miradi ya ujenzi inayotekelezwa kwenye wilaya hiyo kama ubora wake unalingana na thamani halisi.

“Baada ya kupata majibu ya uchunguzi na kubaini kiini cha tatizo ndani ya wilaya hii hatua zitachukuliwa,” amesema

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Awali, Mbunge wa Malinyi (CCM), Dk Haji Mponda alimweleza Waziri Mkuu kwenye wilaya hiyo kuna matatizo ya mahusiano kati ya Serikali na Halmashauri jambo linalosababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Mbunge huyo amesema kutoelewana kwa viongozi wa wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumesababisha mgawanyo mkubwa kuanzia katika Baraza la Madiwani hadi kwa wananchi mitaani, hivvyo alimuomba Waziri Mkuu awasaidie  kilipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu  amesema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekani wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao kwa njia ya mabango, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu katika mabango yao hakuna hoja hata moja inayomuhusu Waziri Mkuu zote ni za ngazi ya halmashauri.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

Awali, alipowasili wilayani Malinyi, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa gharama ya Sh3.9 bilioni. Ujenzi huo ulianza Novemba 11, 2017 na utakamilika Septemba 29, 2019. 

Chanzo: mwananchi.co.tz