Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aanika mageuzi uwekezaji

D67ee7546387bc9c09ca105afe3858e9.jpeg Majaliwa aanika mageuzi uwekezaji

Sat, 17 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaja mikakati ambayo serikali imechukua kuhakikisha wawekezaji wanalindwa na vibali vyao vinafanyiwa kazi bila kutumia urasimu wala rushwa.

Aidha, amewatoa hofu Watanzania kuhusu kuendelezwa kwa Makao Makuu ya nchi, Dodoma kuwa serikali imeweka mfumo mzuri utakaohakikisha miundombinu mbalimbali inajengwa kwa mujibu wa sheria ya mipango ya maendeleo ya Jiji la Dodoma.

Wakati huo huo, amesema serikali inafanyia tathmini mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kuangalia namna bora ya uendeshaji wake.

Aliyasema hayo jana bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge kuhusu hotuba yake ya bajeti kwa taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Waziri Mkuu alisema katika masuala ya wawekezaji watafanya mabadiliko ya sera na sheria zake ikiwemo kufanya mabadiliko ya masharti mbalimbali kuhusu vibali vya kazi kwa wawekezaji.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliielekeza ofisi hiyo kuimarisha huduma za pamoja, kushughulikia malalamiko yote kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamaisha uwekezaji kupitia mazungumzo, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maeneo yote ya uwekezaji.

Alisema baada ya maagizo hayo, tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa zikiwamo kuandaa muundo wa wizara ambao utaainisha majukumu ya mgawanyo wa idara na taasisi zitakazokuwa chini ya eneo la uwekezaji.

Alisema wanapitia upya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 kubainisha maeneo yenye uhitaji wa maboresho ambapo tayari tathimini ya utekelezaji wa sera ya taifa imekamilika.

“Pia tunaandaa mkakati wa kitaifa wa maendeleo ya uwekezaji ili kuimarisha utaratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa mausala ya uwekezaji katika sekta zote nchini,” alisema Majaliwa.

Alisema kukamilika kwa hatua hizo kutaiwezesha serikali kutekeleza masuala muhimu kama kushiriki kikamilifu katika mikutano na majadiliano ya jumuiya kikanda yanayohusu masuala ya uwekezaji yakiwemo maandalizi ya Sera ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alieleza kuwa serikali itajenga mazingira rafiki ya wawekezaji na uchumi shindani nchini na kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha mazingira hayo.

Alieleza kuwa katika kuhakikisha hali ya uwekezaji inaimarika, wameandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wawekezaji pamoja na kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara ambalo linaundwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na taifa ambalo mwenyekiti ni Rais.

Aidha, aliagiza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ziibuliwe na wananchi waelimishwe namna ya kupata wabia ili kushirikiana nao, pia kuimarisha mifuko ya kutoa cheti cha ushiriki wa miradi ya maendeleo.

Aliwakumbusha watendaji wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu kuhakikisha

kuwa muundo na mifumo ya masuala ya uwekezaji inafanyika kazi ndani ya muda uliowekwa na Rais.

“Nasisitiza kuwa watendaji wajiepushe na uombaji wa rushwa, urasimu usiotakiwa katika kuwahudumia wawekezaji ili kujenga imani baina ya serikali au sekta ya umma na sekta binafsi ili tuweze kuzungumza lugha moja,” alisema.

Alisisitiza kuwa mwaka ujao wa fedha 2021/22 serikali itaimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ikiwemo kuanisha ardhi ya uwekezaji na kuendeleza miundombinu muhimu ya uwekezaji katika mikoa yote ili kuvutia uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na migogoro ya mipaka ya utawala kati ya vijiji na vijiji na wilaya na wilaya hata mkoa na mkoa, lakini akieleza mgogoro wa Wilaya ya Kiteto unatakiwa kupatiwa ufumbuzi.

Aliwataka wakuu wa mikoa ya Manyara na Tanga na wa wilaya za Kiteto na Kilindi kumaliza mgogoro huo kabla hajarudi huko.

Chanzo: www.habarileo.co.tz