Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aamsha watendaji mbuga ya Serengeti

0a383ecec89330c831b9ccf458629b99.jpeg Majaliwa aamsha watendaji mbuga ya Serengeti

Sun, 30 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara na watendaji katika sekta ya utalii wabadilike na waweke mkakati wa kuitangaza Mbuga ya Serengeti kuweza kuvutia zaidi watalii na kuitambulisha.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wa nchi na watu na mwongozo huo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuvutia uwekezaji na kuimarisha biashara.

Alitoa agizo hilo juzi wakati akizindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mara mjini Musoma. Aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kuhakikisha watendaji, wataalamu na wananchi wanakuwa nyenzo ya kurahisisha kazi ya kuvutia uwekezaji.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hakikisha watendaji wote wa mkoa wanausoma na kuuelewa ipasavyo mwongozo huu. Hakikisha watendaji wako wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

Waziri Mkuu alisema mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji ambazo endapo zitatumika vema, zinaweza kuipaisha nchi kimaendeleo.

“...Nitoe mwito kwa uongozi mzima wa mkoa uhakikishe unaratibu vilivyo shughuli za uzalishaji hasa wa malighafi, bidhaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya wananchi na mahitaji ya viwanda vya ndani,” alisema.

Alisema miongoni mwa maeneo ambayo Mkoa wa Mara unaweza kunufaika zaidi kwenye uwekeza- ji kutokana na fursa zilizopo ni kilimo, mifugo na uvuvi.

Serikali ilitoa maelekezo yenye lengo la kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuzalisha malighafi za kutosha zitakazotumika kwenye viwanda.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Uwekezaji kushirikiana na mkoa kuwezesha Kituo cha Uwekezaji cha Kanda (TIC)

kilichopo mkoani Mwanza kuanzisha Kituo cha Kutolea Huduma kwa Pamoja ambacho kinapaswa kuwa na rasilimali za kutosha, vifaa na wataalamu wote muhimu.

Alitaja wataalamu wanaopaswa kuwapo ni wa Ardhi, Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Vipimo, NEMC, Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa.

Aliagiza pia idara zote za kisekta katika ngazi ya mikoa na wilaya, zishirikiane katika kubuni njia rahisi zitakazosaidia kuondoa urasimu na kurahisisha uwekezaji katika maeneo yao ili kuongeza ajira na vyanzo vya mapato ya serikali.

“Viongozi na watendaji wa sekta ya umma, fanyeni vikao na sekta binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ili kujadili na kutatua kero za kibiashara na uwekezaji zinazowakabili kwa wakati,” alisema.

Majaliwa alizitaka mamlaka husika zihakikishe zinaweka mipango ya urasimishaji sekta isiyo rasmi, kurasimisha namba msimbo, kuwapatia wafanyabiashara ndogo maeneo ya kufanyia biashara na kuongeza kasi ya upimaji ardhi na kasi ya utekelezaji wa anuani za makazi na postikodi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuchochea fursa za kibiashara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz