Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aagiza wanaostahili kwenda shule wawe darasani

Fbadaab6e1d235366471c0bc5645ae6e.jpeg Majaliwa aagiza wanaostahili kwenda shule wawe darasani

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote za wilaya nchini kusimamia kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shuleni wanakuwa shuleni, huku akisisitiza kuwa endapo katika halmashauri yeyote atakutwa mtoto anafanya biashara badala ya kuwa darasani, viongozi wake watawajibika.

Aliyasema hayo Dar es Salaam jana kabla ya kuzindua ugawaji wa magari kwa maofisa elimu wa shule za msingi wa wilaya zote 184 nchini uliofanyika katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Alitoa onyo kwa halmashauri zote kuhakikisha zinatunza magari hayo kwa kuyapatia huduma za matengenezo na endapo halmashauri itazembea na kuacha magari hayo yaharibike, itawajibika.

Alisema suala la utoaji wa elimu ni jukumu la serikali hivyo ni jukumu la watendaji kuhakikisha wale wote wanaostahili kwenda shule wanakwenda shule.

“Waliofaulu darasa la saba ni lazima kwenda shule, na waliofaulu kidato cha nne ni lazima kwenda kidato cha tano. Hii ni amri ya serikali na wala si uamuzi au hiari ya mzazi. Tutawachukulia hatua wazazi wanaozuia watoto wao kwenda shule,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alizitaka halmashauri hizo kuandaa mipango itakayozuia watoto wa shule kufanya biashara mitaani katika vituo vya mabasi hususani vituo vipya vilivyojengwa katika mikoa kadhaa nchini.

“Hakuna mtoto kukaa nyumbani, itakuwa ni kosa kwa mkurugenzi endapo atakamatwa mtoto wa umri wa shule akifanyabiashara mtaani au vituoni,” alisisitiza.

Aliwataka viongozi waliopo katika halmashauri hizo nchini kushughulikia kwa nguvu zote tatizo la utoro lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtoto anayeanza shule anamaliza.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Washirika wa Maendeleo na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa.

Kuhusu makabidhiano ya magari hayo 184 kwa halmashauri za wilaya, alizitaka halmashauri zilizopokea magari zizingatie taratibu za serikali katika matumizi na matengenezo ya magari hayo.

“Magari haya mmekabidhiwa, maafisa elimu na wakurugenzi wa Halmashauri, tukute gari limepaki kisa limekosa 'service' utakuwa umekosa kazi, lazima tuambizane ukweli, magari haya lazima yafanye kazi kwa zaidi ya miaka mitano hadi sita,” alisisitiza.

Alisema magari hayo ni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa maofisa elimu, na yametolewa na serikali ili yasaidie kuharakisha shughuli za utekelezaji wa majukumu katika sekta ya elimu.

Aidha, aliwataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuchukua hatua ikiwa magari hayo yatatumika tofauti na malengo yaliyotarajiwa. “Hakikisheni magari haya yanakwenda kutekeleza shughuli za elimu kwenye halmashauri zenu na si vinginevyo,” aliagiza.

Pia, aliwaagiza maofisa elimu na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kila kwenye shule ya sekondari wanakamilisha ujenzi wa maabara ili kila shule ipatiwe vifaa vya maabara.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu alisema magari hayo yamenunuliwa na serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Sekta ya Elimu (EP4R) kwa gharama ya Sh bilioni 16.4.

Ummy alisema hiyo ni awamu ya pili ya ununuzi wa magari baada ya awamu ya kwanza ambayo magari 26 yalinunuliwa kwa ajili ya usimamizi wa elimu katika ngazi ya mikoa.

Alisema awamu ya pili ya ununuzi wa magari 184 yatakabidhiwa kwa maofisa elimu wa shule za sekondari kwa ajili ya matumizi ya shule hizo.

Alieleza kuwa kupitia programu hiyo ya EP4R fedha hutolewa kwa kukidhi vigezo ambapo serikali ilikidhi vigezo hivyo baada ya uhakiki kukamilika na hivyo kupatiwa jumla ya Sh bilioni 166.5 katika mwaka wa fedha 2021.

Alisema fedha hizo zilitumika katika ununuzi wa magari hayo 184, ujenzi wa majengo ya elimu, matundu ya vyoo, mabweni kwa shule za msingi na sekondari, ukarabati wa shule kongwe tano na kujengwa shule mpya kumi za sekondari ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.

“Huu ni mwendelezo wa jitihada za serikali katika kuboresha elimu. Pia tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya sekta ya elimu. Zitatumika kuhamisha walimu kutoka shule zenye wanafunzi wachache kwenda kwenye zenye wanafunzi wengi,” alieleza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz