Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aagiza tanzanite iuzwe Mirerani tu

30ea3d781e520d1b5757a52a9ca17bd4 Majaliwa aagiza tanzanite iuzwe Mirerani tu

Thu, 8 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Madini ihakikishe biashara ya madini ya tanzanite inafanyika Mirelani, wilayani Simanjiro katika Mkoa wa Manyara na si mahali pengine popote.

Pia ametoa miezi mitatu kwa wanunuzi wa tanzanite waliopo Arusha na maeneo mengine kujenga ofisi zao Mirelani na wahamie huko.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizindua Kituo cha tanzanite cha Magufuli kilichopo Mirelani.

Majaliwa alisema kitendo cha nchi nyingine kutangaza kuzalisha tanzanite kinaondoa heshima ya Tanzania na uhalali wa kumiliki madini haya ambayo yanapatikana Tanzania pekee.

“Nawaagiza Wizara ya Madini, biashara yote ya tanzanite ifanyike hapa Mirelani, michakato yote ya tanzanite iishie hapa, lengo letu serikali ni kuifanya dunia itambue kwamba tanzanite inazalishwa Tanzania tu. Tumefanikiwa kutangaza jina la tanzanite sana lakini hatujafanya vya kutosha kuifanya dunia itambue tanzanite ni mali ya Tanzania na inatoka hapa Mirelani,”alisema Majaliwa.

Aliiagiza Wizara ya Madini ihakikishe hadi Julai 10 mwaka huu wawe wamebadilisha kanuni zao ili wanunuzi wa tanzanite wote wahamie Mirelani.

"Natoa miezi mitatu watu wajenge ofisi zao hapa na lazima tuweke utambulisho kwenye madini yetu ya tanzanite, hatuna muda wa kubembelezana, tunataka uchimbe madini hapa, makadirio yafanyike hapa na uchakataji ufanyike hapa,”alisema Majaliwa.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, alisema jengo hilo limejengwa na Mkandarasi SUMA JKT kwa gharama ya Sh bilioni 1.4 na lilikamilika tangu Februari mwaka jana.

Profesa Msanjila alisema mradi wa kufunga umeme na taa kuzunguka ukuta wa Mirelani uligharimu Sh milioni 716.5 na gharama ya kusimika mfumo wa kamera za CCTV uligharimu Sh bilioni 1.4 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kuzunguka ukuta wote.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kabla ya kujenga ukuta huu mwaka 2016/2017 zilizalishwa kilo 312.3 za tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 4.2 na serikali ilipata mapato ya shilingi milioni 238, lakini baada ya kujenga ukuta mapato yaliongezeka kwa mfano mwaka jana zilizalishwa kilo 2,186 za tanzanite yenye thamani ya shilingi bilioni 20.3 na serikali ilipata mapato ya shilingi bilioni 1.5,”alisema.

Alisema jengo hilo lina ofisi mbalimbali ikiwemo Uhamiaji, Tume ya Madini Mkoa, TRA, Polisi, benki, uthaminishaji madini na utunzaji madini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula alisema mchango wa sekta ya madini kwa pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia nne hadi asilimia saba baada ya kufanyika kwa mageuzi katika sekta hiyo kuanzia mwaka 2017.

Imeendikwa na Veroni Mheta, Manyara na Matern Kayera, Dar

Chanzo: www.habarileo.co.tz