Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aagiza kilimo cha alizeti kusimamiwa

36637105744b540190cb5f6e79adcdea.jpeg Majaliwa aagiza kilimo cha alizeti kusimamiwa

Mon, 14 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, maofisa kilimo na maofisa ushirika washirikiane kusimamia kilimo cha alizeti ili nchi iache kuagiza mafuta ya kula kutoka nje.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa, Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na wadau wa zao la alizeti kwenye ukumbi wa kituo cha mafunzo cha Kanisa Katoliki, mkoani Singida.

Alisema hakuna sababu ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa sababu nchi ina ardhi nzuri pamoja na nguvu kazi ya kutosha kuzalisha zao hilo.

“Lengo la serikali ni kuongeza uzalishaji na tija kwa kuimarisha utafiti, huduma za ugani, upatikanaji wa mbegu bora na viuatilifu, kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo, kuwajengea uwezo wazalishaji kuhusu kanuni za kilimo bora, kuanzisha mfumo imara wa ugharamiaji wa mazao ya mafuta kwa kushirikisha taasisi za fedha,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Ni matarajio ya serikali kuwa mikakati hiyo itawezesha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 649,437 hadi tani 1,500,000 za alizeti zitakazochangia upatikanaji wa mafuta kwa takribani tani 300,000 ifikapo 2025. Pia serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija.”

Alisema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa tani 650,000 na uzalishaji wa ndani ni wastani wa tani 290,000 sawa na asilimia 45 ya mahitaji kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania huagiza wastani wa tani 360,000 hadi tani 400,000 za mafuta ya kula kufidia upungufu huo na kugharimu takribani Sh bilioni 474 kwa mwaka.

“Fedha hizi ni nyingi, kama tungelikuwa tunajitosheleza katika uzalishaji wa mafuta hapa nchini zingeokolewa na kuelekezwa kwenye maeneo mengine ikiwamo uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu,” alisema Majaliwa.

Alisema serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwamo ya chikichiki, alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz