Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini, zihakikishe ujenzi wa vyumba vya madarasa unakuwa endelevu, kwa sababu idadi ya wanafunzi walioandikishwa na wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, inafahamika kupitia mitihani ya majaribio.
Alitoa agizo hilo jana baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Buhongwa iliyoko Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu ikiwemo madarasa.
”Ni lazima mtoto wa Kitanzania aliyefaulu aende sekondari, jukumu la halmashauri ni kuhakikisha inajenga vyumba vya kutosha vya madarasa. Ifikapo Februari 28, 2021 ujenzi wa vyumba vya madarasa uwe umekamilika na kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kuingia darasani,” alisema.
Pia, Waziri Mkuu aliwataka walimu waendelee kufanyakazi kwa bidii na kwamba serikali inatambua na kuthamini kazi nzuri wanayoifanya, ambayo inawezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu kila mwaka.
Hata hivyo, Majaliwa aliwataka wanafunzi hasa wa kike wahakikishe wanatimiza ndoto zao kielimu na wasikubali kurubuniwa. “Lazima mtoto wa kike alindwe ili aweze kutimiza ndoto zake na serikali imetunga sheria kali kwa atakayewakatisha masomo,” alisema.
Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema jiji hilo tayari limejenga vyumba 67 na wamejipanga kukamilisha ujenzi wa vyumba 53 ili kufikisha vyumba vya madarasa 120 vinavyohitajika ili ifikapo Januari 11, 2021 watoto waliofaulu waanze masomo.
Akizungumzia kuhusu hali ya ufaulu katika jiji hilo, mkurugenzi huyo alisema kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu Halmashuri ya Jiji la Mwanza imeshika nafasi ya tatu kitaifa na Shule ya Mazoezi Butimba B imekuwa ya kwanza kwa shule za serikali Kitaifa. Ufaulu ulikuwa asilimia 98.1.
Alisema katika shule ambazo zinaendelea kujengwa, wamepeleka matofali 6,000 kila shule na mifuko ya saruji 200 ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa. Matofali hayo yanatengenzwa katika kiwanda cha halmashauri ambacho kimeanzishwa kwa ajili ya ufyatuaji wa matofali, wanayoyatumia kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya.