Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema wanafunzi wakiwemo wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini China waliozuiwa kwenda vyuoni kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, sasa wanasoma kwa njia ya mtandao wakiwa popote.
Ugonjwa huo hadi sasa upo zaidi ya nchi 125 huku watu zaidi ya 129,300 wakipata maambukizi na kusababisha vifo zaidi ya 4,700.
Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi ya Machi 12, 2020 katika mahafali ya 38 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT), katika uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
Akizungumza katika mahafali hayo Majaliwa amesema baada ya virusi vya corona kuikumba China vyuo vyote vilifungwa lakini sasa vimefunguliwa na wanafunzi wanasoma kwa njia ya mtandao
“Tehama sasa imefikia katika hatua nzuri kwa sababu Mhadhiri mmoja anaweza kuwafundisha wanafunzi wake wote popote walipo kwa njia ya mtandao. Tehama imewezesha wanafunzi waliozuiwa kurudi nchini kutokea China kuendelea na masomo wakiwa nyumbani kwao,” amesema.
Waziri Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwataka wahitimu wa CKHT kuelewa kuwa vyeti walivyotunukiwa ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha katika masomo yao, hivyo wanaporejea kwenye jamii wahakikishe wanaipatia tuzo ya utendaji bora.
Pia Soma
- Tanzania yapongezwa kudhibiti dawa za kulevya
- Waziri Ikupa awafunda wanawake walemavu
- Tanzania kuadhimisha wiki ya maji bila wageni kutoka nje, corona yatajwa
- VIDEO: Mchungaji Msigwa atoka jela
“Hakikisheni mnaonyesha tofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania kuhusu mustakabali mzima wa kujiletea maendeleo,” amesema Majaliwa.
Amesema amefuatilia kwa karibu maelezo ya viongozi waliotangulia kuhusu umuhimu na hata mafanikio ya chuo hicho, amewataka watambue kwamba Serikali inakiangalia kwa jicho la karibu kwa kuwa kimekaa kimkakati zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Ili kuboresha utendaji wa chuo hicho, Majaliwa ametoa rai kwa uongozi wa CKHT na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TVV) kuhakikisha udahili wa CKHT unatanuliwa kwa sababu hadi sasa chuo kina kozi moja tu ya maandalizi kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuingia kwenye shahada.
Waziri Mkuu amesema katika kuongeza udahili kwenye elimu ya juu, ameshauri wawe na kozi ama programu za maandalizi kwa wale wanaotaka kusoma stashahada na kwa wale wa cheti pia.
Amesema matokeo ya programu hizo yataongeza ushiriki wa Watanzania wengi kwenye elimu ya juu.
“Wito wangu kwa TCU nchini kuhakikisha inasimimia na kuongoza, kwa kushirikiana na CKHT katika uanzishwaji wa programu hizi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora wa elimu ya juu,” amesema.
Katika mahafali hayo, wahitimu 698 walitunikiwa vyeti wakiwemo 20 wa shahada za uzamivu na wengine 185 shahada na stashahada za uzamili, wengine 344 walitunukiwa shahada, 166 walitunikiwa stashahada na astashahada mbalimbali.