Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Wakazi wa Kondoa chagueni CCM

9956f6dfcd4670a7c7323dc035549b4f Majaliwa: Wakazi wa Kondoa chagueni CCM

Tue, 15 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba wananchi wa Kondoa kuwaamini na kuwachagua viongozi wanaoletwa na CCM ili wachochee maendeleo zaidi.

“Endeleeni kuiamini serikali hii ili iendelee kuongoza, endeleeni kuwaamini viongozi wanaoletwa na CCM ili waendelee kuleta maendeleo zaidi. Ninaomba kura za Mheshimiwa Rais, wabunge na madiwani watarajiwa wa CCM sababu ndio wataleta maendeleo katika maeneo yenu,” alisema.

Alitoa mwito huo wakati akizungumza na wananchi wa Kondoa Mjini na Vijijini waliofika kusikiliza sera za wagombea katika uwanja wa SabaSaba, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.

Aliwaombea kura wagombea ubunge wa Kondoa Mjini, Ally Makoa na Dk Ashatu Kijaji wa Kondoa Vijijini na wagombea udiwani. Alitoa mwito kwa wananchi kutumia kipindi hiki kutafakari kwa kina na kuchagua viongozi wanaowafaa.

“Wananchi msiyumbe, tuna uchaguzi wa aina mbili. Uchaguzi wa kwanza ni kuchagua kiongozi anayeweza kuleta maendeleo na mwenye uwezo wa kuleta maendeleo na uchaguzi wa pili ni uchaguzi wa kishabiki wa kufuata upepo.”

“Tutumie kipindi hiki kuchagua viongozi wanaoweza kutusemea masuala ya maendeleo,” alisema.

Akielezea miundombinu ya barabara, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami na hata katika baadhi ya wilaya huku akitolea mfano wa kutoka Babati hadi Kondoa, Kondoa hadi Chemba na Chemba hadi Dodoma.

“Sasa hivi tunataka kufungua barabara ya kutoka Babati hadi Orkesumet, na hii ya kutoka Handeni - Kiberashi – Kondoa – Singida iko kwenye ilani yetu ya sasa ukurasa wa 73. Barabara hii ikitoka Handeni itapita Kilindi – Kiteto – Kondoa hadi Singida.”

Katika barabara za wilaya, Majaliwa alisema hizo zinashughulikiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ambao wamepewa Sh bilioni 1.840 na Sh bilioni 6.4 nyingine zilitolewa kwa ajili ya barabara za Kondoa Vijijini kutoka makao makuu na kuunganisha kata hadi kata.

Kuhusu mikakati ya serikali kukuza uchumi, alisema kuna watu wanabeza ujenzi wa reli na ununuzi wa ndege, lakini wanasahau kuwa maendeleo ya watu hayaji bila maendeleo ya vitu.

“Huwezi kupata maendeleo ya watu bila kuwa na maendeleo ya vitu,” alisisitiza. Katika sekta ya kilimo, Majaliwa alisema wananchi wa Kondoa ni wakulima wazuri wa mazao mbalimbali na akawakumbusha wakazi hao jinsi serikali inavyoboresha upatikanaji wa mbolea na pembejeo za kilimo.

“Kilimo ndicho kinasheheneza mkakati wetu wa uchumi wa viwanda. Mpaka sasa, tumeshaanzisha viwanda 8,477 na hapa nasisitiza kuwa, viwanda hivi na miradi ya kimkakati vimesaidia kuongeza ajira nchini,” alisema.

“Lazima niwaeleze ukweli, mkikaa kusubiri ajira rasmi, nafasi ni chache mno. Ukitaka kazi huko halmashauri au kwingineko, itabidi usubiri hadi waliopo wastaafu.

Ndiyo maana tumeanzisha miradi ya kimkakati ya reli ya kisasa, mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere na mingine ili wananchi waweze kupata ajira huko,” alifafanua.

“Vijana wanaojiajiri kwenye ususi, kuchomelea nondo, wafanyabiashara ndogo wote hawa wana ajira. Ajira siyo lazima iwe ile ya kushika kalamu ofisini,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz