MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa amesema mafundisho na miongozo ya viongozi wa dini ni sababu kubwa inayoiwezesha Tanzania iendelee kuwa na amani.
Alisema hayo baada ya kufungua msikiti wa Rahman katika kijiji cha Kwamndolwa wilayani Korogwe, Tanga.
Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea taifa na akasema Watanzania wanapaswa kuendelea kuwarithisha imani za dini watoto ili kuwajenga katika misingi ya maadili wawe raia wema.
Aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuliombea taifa tangu mchakato wa Uchaguzi Mkuu ulipoanza.
"Tunawashukuru viongozi wa dini, tuna zaidi ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa kampeni na bado amani inaendelea kutawala nchini, hivyo msichoke kuliombea Taifa na kuwaombea wote wanaoshiriki katika mchakato wa kampeni."
Msikiti huo umejengwa kwa gharama ya sh. milioni 150 kwa ufadhili wa taasisi ya Firdausi ambayo imekuwa ikijenga misikiti, kutoa misaada na kuchimba visima kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Ufunguzi huo ulihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir bin Ally, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa na wakazi wa Kwamndolwa.