Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mji wa Serikali uliopo Ihumwa Kilomita 17 kutoka Dodoma mjini na kutoa maagizo 14 yatakayoharakisha kukamilika kwa kazi hiyo.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Januari 16, 2019 mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Ihumwa lililopo kilomita 17 kutoka Dodoma mjini.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu amesema pamoja na spidi anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora.
“Kazi ya ujenzi ikamilike Januari 31, 2019 kwa kasi na viwango vyenye ubora kuanzia mifumo ya ICT, umeme na maji izingatiwe wakati wa ujenzi na zile sites zenye upungufu wa nguvu kazi, vijana waongezwe na kazi ifanyike mchana na usiku,” amesema na kuahidi kurudi Januari 31 ili kukabidhiwa funguo za ofisi zote za wizara.
Amewataka waratibu wa zoezi la Serikali kuhamia Dodoma wakiwemo Wizara husika na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe kuwa wakandarasi ambao hawajalipwa hususan vikosi vya ujenzi wanaojenga jengo la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wanalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wahakikishe wanafungua ofisi ya muda katika mji wa Serikali ili kurahisisha usimamizi wa miundombinu inayowahusu.
Ametumia fursa hiyo kuwataka Wakala wa Majengo nchini (TBA) wawasilishe taarifa ya maendeleo ya ujenzi kwa kila wizara kwa kila hatua inayoendelea.
Akihitimisha, Waziri Mkuu alisema Ofisi ya Waziri Mkuu ipatiwe taarifa ya idadi ya ajira iliyotengenezwa kutokana na ujenzi wa mji wa Serikali hususan za wale ambao hawana ajira za kudumu kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi huo.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi huo, katibu wa kamati ya kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe alisema ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja umegharimu Sh3.6 bilioni na uko kwenye hatua za mwisho.