Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Tutaongeza ukusanyaji mapato

53562c8a8ce6952bfefc11b496ced03f Majaliwa: Tutaongeza ukusanyaji mapato

Sun, 14 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itatekeleza mikakati mahususi ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ambayo ni pamoja na kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa halmashauri na serikali za mitaa.

Pia, waziri mkuu amesema serikali itaimarisha ushirikiano kati ya mamlaka zinazokusanya mapato na vyombo vya ulinzi na usalama, katika kufanya doria maeneo ya mipaka ya nchi kavu, baharini na kwenye maziwa ili kudhibiti biashara za magendo.

Alisema hayo jana wakati akiahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 12 Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa “ pia serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanatumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD).”

Kuhusu mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka huu 2020/2021, Majaliwa alisema serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 55,287 na pia itaendelea kuzingatia kigezo pekee cha uhitaji wa mwombaji sanjari na kurahisisha matumizi ya mtandao katika uombaji na utoaji wa mikopo.

Alisema katika kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, serikali imefanya maboresho ya kisheria, kimfumo na kiutendaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015/2016 – 2019/2020).

Majaliwa alisema matunda ya maboresho hayo ni kuongezeka kwa makusanyo ya fedha za mikopo kutoka wastani wa Sh bilioni 28.9 mwaka 2016/2017 hadi kufikia wastani wa Sh bilioni 192 mwaka 2019/2020.

‘Serikali inafarijika na inapokea kwa mikono miwili michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa na Serikali baada ya miaka 15 ya uwepo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuhusu namna bora zaidi ya kuboresha mfuko huu,” alisema.

Aliagiza kuwa ili mfuko huo uwe endelevu, himilivu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ihakikishe kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaboresha huduma zake na kurahisisha urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika waliojiari katika sekta binafsi.

Waziri Mkuu aliwasihi wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu, ambao bado hawajajitokeza na kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja. Pia aliwataka waajiri wote nchini katika sekta binafsi na sekta ya umma, watoe kipaumbele kwa makato ya mikopo ya elimu ya juu, kama yalivyo makato mengine ya kisheria.

Chanzo: habarileo.co.tz