WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia idadi kubwa ya watumiaji zikiwemo nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aliyasema hayo alipokutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Leonard Chamuriho, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Erick Hamissi, Wakala ya Meli Tanzania (TASAC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kamishna wa Forodha pamoja na wadau wa masuala ya usafirishaji.
Majaliwa alisema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika uboreshwaji wa huduma mbalimbali bandarini zikiwemo za upakuaji wa mizigo.
Waziri Mkuu alisema serikali imejipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mizigo yote inayopitia bandarini inapakuliwa katika kipindi cha muda mfupi.
Alisema bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimefanyiwa maboresho makubwa, hivyo amewasisitiza wadau wa sekta binafsi waendelee kuleta meli za kutosha.
Alisema mbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hizo, pia bandari za Kabwe, Kasanga zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa bandari ya Karema ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika nchi za Congo, Zambia na Burundi.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Chamuriho alisema ujenzi ndani ya Bandari ya Dar es Salaama unaelekea kukamilika.
“Gati zote saba tumezimaliza na sasa tunamalizia eneo la makontena katika gati namba sita na saba ambalo litakamilika mwezi Agosti, 2021, hii itasaidia kuongeza ufanisi ndani ya bandari,” alieleza.
Pia ameongeza kuwa wataendelea kuzingatia masuala yote ya kisheria, kisera, kiutawala na kiutendaji na kuyasimamia kikamilifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa bandari ili kila anayeitumia anufaike.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema shirika hilo limefanikiwa kukarabati mabehewa zaidi ya 200 ya mizigo ambayo yanaenda nchi za Burundi na Congo.
Kadogosa alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali imelitengea shirika hilo bajeti kukarabati mabehewa 660 na kazi ya ukarabati itaanza muda wowote, pia vichwa vingine tisa vitakarabatiwa ili kusafirisha mizigo.
Akizungumzia kuhusu usafirishaji wa mafuta nchini Uganda, Kadogosa alisema wameanza kutekeleza kazi hiyo ambayo ilikwama kwa takribani miaka 15 na wiki ijayo watapeleka lita milioni moja kwenda nchini Uganda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wa sekta ya bandari wameipongeza serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua kuboresha sekta hiyo na wameshauri hatua zaidi zichukuliwe ili kuvutia zaidi watumiaji wa bandari nchini.