Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Tukitangaza mishahara bei zinapandishwa

87f0e42627fb095228e4148860d0d660 Majaliwa: Tukitangaza mishahara bei zinapandishwa

Fri, 12 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imesema imekuwa ikiboresha maslahi ya wafanyakazi bila kutangaza kwa kuwa ikitangaza bei ya bidhaa zinapanda na kuongeza ugumu wa maisha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (ACT-Wazalendo) wakati wa kipindi cha Maswali cha Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.

Aliwaeleza wabunge kuwa serikali inatambua mchango wa wafanyakazi kwa kuwa inapata mafanikio kupitia wao, ndio maana inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuongeza maslahi yao ambayo pia mengine yanakua hata zaidi ya mishahara.

Katika swali, Haji alisema miongoni mwa ahadikatika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupitia kauli za Rais John Magufuli ni pamoja na uboreshwaji wa maslahi ya wafanyakazi.

“Mheshimiwa wafanyakazi wa Tanzania wameendelea kuwa wavumilivu na wastahimilivu na wakijenga matumaini juu ya ahadi hii muhimu katika maisha yao. Je, serikali inatoa kauli gani na ni lini wafanyakazi wa Tanzania watapandishiwa mishahara yao na kuboreshewa maslahi yao?,” alihoji.

Waziri Mkuu alisema serikali ina dhamira ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kupitia eneo la mishahara lakini pia upandishwaji wa madaraja na maeneo mengine.

Alisema Serikali Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilijifunza kwamba wakati inapotangaza kupandisha mishahara, husababisha ongezeko la gharama kwenye masoko na kusababisha ugumu wa maisha ya wengine.

“Tunao wafanyakazi lakini tunao wakulima, tunao wafugaji lakini tunao wavuvi hayo ni makundi mbalimbali lakini kwa eneo la wafanyakazi pekee yake, ukitangaza hadharani kwamba tumepandisha mishahara kwenye masoko yetu, vituo vya mabasi na huduma zingine zote bei zinapanda,” alisema.

Alisema kupandishwa kwa bidhaa na huduma hizo kunafanyika kwa sababu ya maslahi ya kundi moja huku makundi mengine yakiwa hayana uwanja wa kupandishiwa maslahi.

“Kwa hiyo tumeona kwenye eneo hili tutumie njia ambayo si lazima tutangaze hadharani lakini tunaboresha maslahi ya wafanyakazi. Maslahi ya wafanyakazi hayako kwenye mishahara tu, tunapandisha madaraja na tunapunguza kiwango cha kodi lakini pia kuna namna mbalimbali za kumfanya mtumishi aweze kupandishiwa maslahi yake,” alisema.

Alikiri kuwa wafanyakazi wengi wanasubiri kusikia kupanda kwa mishahara na kusisitiza kuwa kutangazwa kupanda kwa mishahara kunaongeza ugumu wa maisha.

“Bado serikali inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuongeza maslahi ya watumishi ambayo pia mengine yanakua hata zaidi ya mishahara,” alisema.

Alisema Rais Magufuli mara kadhaa kupitia sherehe za wafanyakazi amekuwa akisema kupandisha mishahara kwa Sh 20,000 au Sh 30,000 haina tija kama pale serikali ikiamua kupunguza kodi ambayo mfanyakazi anakatwa.

“Kupunguza kodi kutoka kwenye double digit kwenda kwenye single digit lile ongezeko linaweza kuwa kubwa zaidi kuliko hili la kupandisha mshahara wa Sh 10,000 na kuendelea,” alisema.

Alisema pia, Rais pamoja na serikali ameendelea kuahidi kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.

“Bado serikali ipo na imeingia madarakani tunatambua mchango mzuri sana unaotolewa na watumishi wa umma na serikali yao inatambua inapata mafanikio kwa sababu ya mchango wao mkubwa,” alisema Waziri Mkuu.

Alitoa wito kwa watumishi wa umma wasikate tamaa wakidhani kutangazwa mshahara hadharani ndio kunaweza kutatua matatizo.

Chanzo: habarileo.co.tz