Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Serikali inathamini dini, sekta binafsi

3b5d18b31e1d5d45ac3087ab6a5e99a5 Majaliwa: Serikali inathamini dini, sekta binafsi

Mon, 5 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi na taasisi za dini likiwemo Kanisa Katoliki katika kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Majaliwa alibainisha hayo jana Jumapili alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu katika Ibada ya Kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, Askofu Simon Chibuga Masondole.

Ibada hiyo ilifanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu Bunda, Mkoani Mara.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini katika kutoa huduma hizo kwa Watanzania wote bila ubaguzi wowote.

"Upo usemi usemao ‘Kama unataka kwenda haraka tembea peke yako, lakini kama unataka kwenda mbali tembea na wenzako.’ Sisi wote tuna imani kubwa nawe kuwa utaendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo baina ya Serikali na Kanisa," alisema

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kutumia nyumba za ibada kuliombea Taifa ili waendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano.

"Amani tuliyo nayo, ndio chachu kubwa ya kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi," alisema

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Hapi alisema wataendelea kutoa ushirikiano usio na mashaka kwa Askofu Masondole kwa kuwa wanatambua mchango wa Kanisa hilo katika mkoani Mara.

Chanzo: www.habarileo.co.tz