Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Ndoto za JPM zitumike kupaisha uchumi

87884bd7ea3f43f7c2111ea1c4fd0597 Majaliwa: Ndoto za JPM zitumike kupaisha uchumi

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa vipaumbele vyote ambavyo havikukamilika katika kipindi kilichopita na kusimamia ipasavyo maeneo mapya yaliyoibuliwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 na Hotuba ya Rais wakati akizindua Bunge la 12.

Aidha, amewahimiza wabunge kutumia fursa ya ndoto za Rais John Magufuli za kuona Tanzania inajenga uchumi imara, kwa kuwa wao ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa na utatuzi wa kero za wananchi.

Waziri Majaliwa aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hoja yake kwa ajili ya wabunge kuanza kujadili hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati akifungua Bunge la 12 ,Novemba mwaka jana.

Alisema katika vipaumbele vinavyotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Rais Magufuli aliweka bayana kuwa mambo yote muhimu yatakayotekelezwa yamebebwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 - 2025.

“Kadhalika, alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutekeleza na kusimamia masuala muhimu aliyoyaeleza kwenye Hotuba yake ya kuzindua Bunge la 11 Novemba 20, mwaka 2015,” alisema.

Alifafanua kuwa, kwa msingi huo, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa ahadi na maelekezo ya Rais aliyoyatoa wakati akizindua Bunge la 12 sambamba na Bunge la 11.

“Nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba baada ya hotuba ya Mheshimiwa Rais kutolewa utekelezaji wa maelekezo yake ulianza mara moja kwenye maeneo mbalimbali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Wizara na Taasisi zote ziliichukua hatua za makusudi kuchambua hotuba hiyo, kuainisha maeneo ya utekelezaji sanjari na kuja na mipango ya utekelezaji wa muda mfupi, muda wakati na muda mrefu,” alisema.

Alisema ni ndoto ya Rais Magufulu kuona Tanzania inajenga uchumi imara, shindani sambamba na kutengeneza ajira za kutosha kwa Watanzania.

Na kutoa rai kwa Wabunge kutumia vema fursa hiyo adhimu. Aliwahakikishia wabunge hao kuwa michango yao itaheshimiwa, itathaminiwa na pia itaifanyiwa kazi kwa lengo la kushughulikia kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Chanzo: habarileo.co.tz