Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Msirubuniwe na makundi hatari kwa usalama

A49b008105e0894a3078278bdacdce3c.jpeg Majaliwa: Msirubuniwe na makundi hatari kwa usalama

Sat, 12 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania hususani vijana wasikubali kurubuniwa na makundi ya watu wasio na mapenzi mema na nchi, ambao watataka kuwatumia kwa maslahi yao binafsi na kuhatarisha usalama na amani ya nchi yao.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, uliofanyika jijini Dodoma. Aliwasisitiza Watanzania wawe wazalendo kwa nchi yao.

"Uzalendo ndio utalifanya taifa liendelee kujitegemea, hivyo ni muhimu suala hilo likapewa kipaumbele. Tusikubali kushawishiwa na Mtanzania yeyote anayetumiwa na watu wenye lengo la kutaka kuja kututawala, tusikubali, lazima tuendelee kuwa huru na tulinde rasilimali kwa manufaa ya wote,"alisema.

Waziri Mkuu alisema uzalendo ni muhimu katika kujenga umoja wa kitaifa na vijana ni zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania, hivyo wakipata misingi mizuri ya uzalendo tutajenga taifa imara, lenye mshikamano, nguvu na kuendelea kudumisha amani nchini.

Alisema serikali kwa kutambua hilo, kupitia Ilani ya CCM 2020-2025 imeweka msisitizo wa kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala ya uzalendo wa kitaifa.

Waziri Mkuu alisema amefurahi kuona skauti wenye umri mdogo katika mkutano huo; na kwamba wanachama wa Chama Cha Skauti huanzia umri wa miaka mitano na kuendelea, ni dhahiri kuwa malezi na makuzi ya uzalendo kuanzia utotoni, yatawezesha ujenzi wa taifa imara lenye wananchi wenye kuipenda nchi yao, kuilinda na kuithamini.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema mlezi wa Skauti Taifa ni Rais John Magufuli na wakuu wa mikoa wote ni walezi wa skauti wa mikoa kwa nafasi zao, hivyo aliwataka wakuu wa mikoa wasiolea Skauti katika maeneo yao wajitathmini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu hao wa mikoa, wahakikishe wanampelekea taarifa ya idadi ya Skauti walioko kwenye mikoa yao na kwamba serikali inahitaji kuona Skauti ikiendelezwa.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka vijana wa Skauti, wazingatie maadili na wawe chachu kwa wengine kuwa na mwenendo mwema.

“Nitoe maagizo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Vijana ahakikishe kwamba masuala ya Skauti yanaingizwa kwenye programu zote za mafunzo kwa vijana. Aidha, mada ya uzalendo ijumuishwe kila yanapotolewa mafunzo mbalimbali kwa vijana mfano mafunzo ya ujasiriamali, urasimishaji wa biashara na upatikanaji wa mitaji," alisema.

Awali, Skauti Mkuu Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza aliiomba serikali iwapatie eneo jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga kambi kuu ya kimataifa, ambayo itakuwa na Chuo cha Ufundi, nyumba ya kulea vijana walioathirika na dawa za kulevya, kituo cha michezo, karakana, hoteli ya mafunzo, maeneo ya utalii na utamaduni, bustani za michezo na mashamba darasa.

Waziri Mkuu alisema serikali iko tayari kuwaunga mkono ili wafanikishe maono yao na hivyo aliielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mlezi wa Skauti katika Mkoa kushirikiana na Chama cha Skauti ili kuhakikisha hicho kinamilikishwa eneo na kuanza kutekeleza mipango iliyotajwa na kuweza kujitegemea kiuchumi.

Chanzo: habarileo.co.tz