Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Mimba za utotoni zitakomeshwa

70e92fbe1e8ce9ea546490e0f945aad3 Majaliwa: Mimba za utotoni zitakomeshwa

Sun, 18 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka tatizo la mimba za utotoni likomeshwa kwani limekuwa sugu nchini.

Majaliwa ameyasema hayo leo Aprili 17, 2021 Mjini Dodoma, katika uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya Uwekezaji katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe.

Majaliwa amesema tatizo hilo linasababisha wanafunzi wengi kushindwa kumaliza masomo yao katika shule za sekondari na msingi akiweka msisitizo kuwa jambo lazima likomeshwe.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40. Tanzania ni asilimia 31.

Kenya ina asilimia 23 wanaoozwa kabla ya kutimiza miaka 18. Majaliwa amesema kuwa Tanzania ina sheria nzuri za kuwalinda vijana na watoto katika makundi tofauti ikiwemo kuwa na sheria kali kwa wanaowapa mimba wanafunzi.

Kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 60A kifungu kidogo cha (3) cha sheria ya elimu namba 353 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 kuwa mtu yeyote atakayempa mwanafunzi ujauzito atakuwa amevunja sheria na atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Aidha Majaliwa amewataka vijana kujitambua na kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia akiwataka wadau kushusha nguvu yao hadi ngazi ya chini Ili watu wapate hudumu.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Doroth Gwajima alisema takwimu zinaonesha bado wasichana wengi wa shule za msingi na sekondari wanaacha shule kutokana na mimba kwa sababu ya malezi duni, lakini pia kujihusisha na mapenzi kabla ya wakati.

“Pamoja na sheria na adhabu zilizopo za kuhakikisha mimba zinakwisha lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu sijui watu hawaogopi?, sijui tuongeze miaka?, bado vitendo hivi vinaongezeka,na nyie vijana achene kujihusisha na mapenzi kabla ya wakati,” alisema Gwajima Alisema Serikali inaendelea kuchambua mila na desturi zinazochangia vitendo vya ukatili wa kijinsia, mimba na ndoa za utotoni ili kuwalinda vijana wa kundi balehe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz