Morogoro. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoboa siri ya kuvunja bodi ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akisema viongozi walikuwa wakimpa taarifa zisizo sahihi kuhusu utekelezaji wa miradi.
Akizungumza wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichopo wilayani Kilosa, Majaliwa alisema alikuwa akipata taarifa kuwa mradi unaendelea vyema, lakini baada ya kutuma wataalamu mbalimbali kutembelea, mradi huo ulionekana kusuasua.
Alisema Serikali ikaamua kuchukua hatua ya kuivunja bodi hiyo pamoja na idara nyingine zilizokuwa zikihusika na mradi huo.
Waziri mkuu alitumia fursa hiyo kuzipongeza bodi mpya ya NSSF na Mkulazi kwa namna zinavyoshirikiana na Jeshi la Magereza katika kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuwafikia wakulima wa nje wa miwa inayotumiwa na kiwanda hicho.
Aliziagiza bodi hizo kufanya jitihada za kutosha kuhakikisha mradi huo unakamilika kama ilivyopangwa.
Sanjari na hilo, Waziri Mkuu alimuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike apeleke wataalamu wengi wa kilimo katika shamba la miwa la Mkulazi ili walisimamie kitaalamu.
Alisema lengo la kuanzishwa shamba hilo la miwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikia kiwango kinachohitajika.
Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee ni kuboresha kilimo cha miwa na kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.
Alisema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na Jeshi la Magereza, hivyo, aliiagiza menejimenti mpya ya Mkulazi kuhakikisha linasimamiwa kikamilifu.
“Tusishindwe na watu binafsi,” alisema.
Mkulazi II ni moja ya mashamba mawili yanayomiilikiwa na wabia wawili, yaani NSSF na Jeshi la Magereza.