Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema maamuzi ya Serikali kuhamia Dodoma yaliyofanywa na Hayati Dk John Magufuli yalikuwa ya kishujaa hivyo Serikali itaendelea kuyaenzi.
Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 25, 2022 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa.
“2016 wakati wa maadhimisho haya Hayati Dk John Pombe Magufuli alitangaza uamuzi wa kishujaa wa kuhamia Dodoma, napenda kuchukua fursa hii kiusisitiza tena kwamba Serikali imedhamiria kwa dhati kuendeleza uamuzi ule kama njia moja ya wapo ya kuenzi maono ya shujaa wetu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema jitihada za kujenga jiji la Makao Makuu ya Taifa zimeendelezwa na Serikali kama ambavyo wananchi wanashuhudia miundombinu mbalimbali ikiendelea kujengwa jijini humo.