Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maagizo 10 ya PM Kassim Majaliwa kuhusu mifugo

Efddab5aa0f3e85081f27c8a7c71a89c.jpeg Maagizo 10 ya PM Kassim Majaliwa kuhusu mifugo

Wed, 8 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo zaidi ya 10 kwa mamlaka za serikali likiwamo la kutekeleza Waraka wa Rais namba moja kwa kutenga asilimia 15 ya mapato yatakanayo na sekta ya mifugo katika halmashauri zitumike kuboresha zaidi sekta hiyo.

Waziri Mkuu pia amekemea tatizo la migogoro baina ya wafugaji na watumiaji ardhi wengine linalosababisha mauaji yanayozuilika.

Alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa sekta ya mifugo nchini.

“Ninatoa maelekezo kwa mamlaka za serikali za mitaa, na leo (jana) wakuu wa mikoa mko hapa, hakikisheni mnatekeleza Waraka wa Rais namba moja wa mwaka 2022 kwa kutenga asilimia 15 ya mapato yatokanayo na mifugo na kuweka katika uboreshaji wa sekta ya mifugo,” alisema. Majaliwa alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kuzisimamia halmashauri zitenge asilimia hizo 15.

Aliwaagiza viongozi na watendaji wa serikali kua karibu na sekta binafsi na wafugaji ili kuwawezesha waendelee kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Pia aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kushirikiana na sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kutenga, kupima, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho.

Alisema mamlaka hizo zina wajibu wa kusimamia wafugaji kuongeza tija katika uzalishaji kupitia uhamilishaji, upandishaji wa madume na mitamba bora.

Aidha, aliitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutumia taasisi za utafiti na kuzipatia fedha zifanye tafiti zenye tija kwa sekta ya mifugo na kuimarisha taasisi zinazozalisha mbegu bora za kisasa pamoja na kuhamasisha wafugaji watumie mifugo bora iliyofanyiwa utafiti na kuonesha kuwa na tija zaidi.

“Pia naagiza wizara isimamie na kuimarisha mfumo wa masoko ya mifugo na wafugaji wauze mifugo yao kwa bei nzuri ikiwamo kuimarisha ushirika wa wafugaji ili wafugaji waweze kufikiwa waunde umoja wao wachanganue changamoto zao badala ya kila mmoja kuwa sehemu yake hivyo kuwa ngumu kuwafikia,” alisema Majaliwa.

Aliiagiza Wizara ya Mifugo kushiriki kikamilifu katika kutatua migogoro inayowahusu wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

“Hakikisheni wafugaji wanaelimishwa na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo. Halmashauri nazo zihamasishe ufugaji ambao hautochochea migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,”alisema Majaliwa.

Aliagiza ng’ombe zaidi ya 5,000 wanaoshikiliwa katika hifadhi mbalimbali nchini, wizara kufuatilia na endapo mahakama imeamuru waachiwe, waachiwe mara moja.

Alitaka pia operesheni za mifugo nchini kufanywa kwa weledi, lakini pia akiwasisitizia wafugaji waepuke shughuli za ufugaji kwenye maeneo yasiyoruhusiwa hususani vyanzo vya maji, hifadhi na maeneo mengine ikiwemo ya kilimo.

Aliagiza mikoa yote kufanya sensa ya mara kwa mara ya mifugo ili kufahamu ipo mingapi na iko wapi.

Alisema sekta ya mifugo ni muhimu na ya kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa na lengo la kuiwezesha kuchangia ipasavyo katika kuwakwamua wananchi kiuchumi na kutoa malighafi ya kwa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.

Majaliwa pia alitoa wito kwa wafugaji kuacha tabia ya kuwapa watoto kazi ya kuchunga mifugo badala yake wajikite katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora kwa manufaa yao ya baadaye.

Aidha, aliwataka kujikita katika ufugaji wenye tija utakaohakikisha malighafi zinazotokana na mifugo kama vile nyama, maziwa na ngozi zinapatikana kwa wingi lakini pia kwa ubora unaoweza kupata soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Alisema kwa sasa uzalishaji wa bidhaa za mifugo bado uko chini kuanzia nyama, maziwa na hususani ngozi ambazo zimeharibiwa na kuwekwa chapa na kuandikwa majina.

“Serikali iko nyuma yenu, hakikisheni mnafuga kwa kuzingatia utaalamu unaotolewa. Rais alitoa maagizo ya kuongeza uzalishaji wa nyama kutoka kilo 730,000 mwaka huu na kufikia 940,000 mwaka 2025/26.

Alisema malengo mengine ni maziwa kuongezeka kutoka lita bilioni 3.1 mwaka huu hadi lita bilioni 4.5 mwaka 2025/26 na ngozi kutoka tani 16 mwaka huu hadi tani 25 mwaka 2025/26.

Alihimiza kuhusu umuhimu wa wafugaji kutumia fursa ya masoko kwa kuwa mataifa mengi yanahitaji nyama kutoka Tanzaia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz