Leo Ijumaa December 15, 2017 Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi imemhukumu aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi, PC George Bisongoza (30), aliyefukuzwa kazi mwaka 2013, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kusafirisha magunia 18 ya bangi yenye thamani ya Sh55.7 milioni.
PC George na mwenzake, walikamatwa katika eneo la Kilema Pofu barabara ya Moshi-Himo, wakisafirisha bangi hiyo kwa kutumia gari la polisi, Toyota Landcruicer.
Hukumu ya kifungo hicho cha maisha, imetolewa leo na Benard Mpepo ambaye ni Hakimu Mkazi mwandamizi mwenye mamlaka ya nyongeza ya kusikiliza kesi kama Jaji.
Akisoma hukumu hiyo Mpepo amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashitaka, haukuacha shaka dhidi ya mshitakiwa kutenda kosa hilo.
Upande wa mashtaka uliongozwa na jopo la mawakili wanne wa Serikali ambao ni Ignas Mwinuka, Verediana Mlenza, Agatha Pima na Vestina Masalu, wakati mshitakiwa akitetewa na wakili Martin Kilasara.
Mpepo amesema mawakili hao walifanya wajibu wao kwa weledi mkubwa kiasi kwamba kila akichambua ushahidi uliotolewa, haoni mahali ushahidi huo unapoweza kumpa mshtakiwa huyo nafuu ya kosa.
Akichambua ushahidi huo Mpepo “amesema siku hiyo usiku, polisi wa doria waliokuwa wanaelekea Marangu, walimkuta mshtakiwa na mwenzake wakiwa na gari hilo la polisi wakitengeneza pancha.”
Kwa mujibu wa ushahidi huo, polisi hao wa Moshi waliwauliza washitakiwa walikuwa wametokea wapi, ambapo waliwaeleza kuwa walitokea Arusha na walikuwa wakimpeleka mzigo wa bosi wao wilayani Rombo.
Hata hivyo, polisi hao hawakuwa na kibali cha kusafiri nje ya Mkoa wa Arusha wala silaha na katika kipindi hicho, polisi wa Moshi walihisi harufu kali ya bangi kutoka katika gari hilo.
Ushahidi huo unaonyesha kuwa gari hilo lilipelekwa kituo cha polisi Himo na baada ya upekuzi, lilibainika kuwa na magunia 18 yaliyosheheni bangi ambapo watuhumiwa ambao ni polisi wakatiwa mbaroni.
Hata hivyo, Mpepo alimwachia huru mshitakiwa wa pili, Livingstone Urassa ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa kijiji cha Kahe huko Rombo, akisema ushahidi uliotolewa haukumgusa mtuhumiwa.
Urassa kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha jela baada ya Mahakama kumtia hatiani Agosti 24 mwaka huu kwa kosa la kukutwa na magunia 16 ya bangi yenye thamani ya Sh49.9 milioni.
Mfanyabiashara huyo alikamatwa baada ya PC George kuwaongoza polisi hadi nyumbani kwake, akidai kuwa gunia 18 walizokutwa nazo kwenye gari la polisi zilikuwa zikipelekwa kwa mfanyabiashara huyo.
Lakini katika hukumu ya leo Ijumaa Mpepo amesema japokuwa ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashitaka unaeleza hadithi hiyo, lakini ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa hamgusi popote.
Baada ya PC George kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha magunia hayo 18 ya bangi, Wakili wa Serikali, Mwinuka aliiomba mahakama itoe amri gari la polisi aina ya Landcruicer PT 2025 lirejeshwe kwa RPC Arusha.
Maombi hayo yalikubaliwa na Mahakama ambapo Mpepo pia aliamuru hukumu na mwenendo huo uchapwe na kukamilika haraka ili akabidhiwe mshitakiwa George kwa hatua za rufaa.
MSIMAMO WA CHUO CHA SAUT MWANZA KUHUSU BINTI ALIEVISHWA PETE NA MWANAMKE MWENZAKE, BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUMTAZAMA