Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lowassa ameacha mzigo wa madeni kwa familia

Lowassa Deaddd).jpeg Lowassa ameacha mzigo wa madeni kwa familia

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Februari 17, 2024, Edward Lowassa alizikwa kijijini kwake, Ngarash, Monduli, Arusha. Ameondoka akiacha utata wa mambo mengi. Kwa jumla yake, huo ni mzigo mzito wa madeni ambao familia yake haina budi kuulipa.

Februari 6, 2008, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchunguzi wa Zabuni na Mkataba wa Richmond na Tanesco, Dk Harrison Mwakyembe, alisoma ripoti bungeni. Ripoti hiyo ilimhusisha Edward kuingilia mchakato.

Katika ripoti hiyo, alikaririwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha, aliyejiita “bangusilo”, kwa maana yeye ni ng’ombe wa kafara, wenye Richmond ni Edward na swahibu wake, Rostam Aziz.

Mipango ya Mungu; Msabaha alifariki dunia Februari 13, 2024. Alifikwa na mauti siku tatu baada ya Edward, aliyeitikia wito wa Mungu Februari 10, 2024. Edward, Msabaha na Nazir Karamagi, walijiuzulu na kuondoka Baraza la Mawaziri Februari 2008.

Februari 10, 2008, Edward alikuwepo Ikulu, Chamwino, Dodoma, Mizengo Pinda, alipoapishwa kuwa Waziri Mkuu. Edward alikuwa na afya njema, imara kabisa. Alimkumbatia Pinda na kumpongeza.

Edward aliendelea na shughuli za kibunge. Baada ya kung’oka uwaziri mkuu, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Alifanya kazi vizuri. Afya ilikuwa imara.

Hata Novemba 2010, Edward alikuwepo bungeni kuapishwa baada ya kutetea jimbo lake la Monduli, Uchaguzi Mkuu 2010. Edward alikuwa na afya timamu. Mwenye tabasamu. Ungesadiki kuwa ni mtu imara. Dhoruba la Richmond halikumtikisa.

Nilikuwepo bungeni kama mwandishi wa habari. Siku Edward aliporipoti bungeni nilimwona. Nilikuwa na kamera, nikampiga picha. Akanifuata, akanyoosha mkono wa kulia, akasema “tisaliamiane kwanza, halafu utaendelea na picha.”

Tukapeana mikono. Aliongozana na Rostam pamoja na wabunge wengine. Kama ambavyo machifu hawatembei peke yao, ndivyo ilivyokuwa kwa Edward. Usingemwona peke yake hata bungeni. Daima aliongozana na watu.Wakati fulani mwaka 2012, Edward alinialika ofisini kwake, Mikocheni, Dar es Salaam.

Hakuwa Edward yule imara. Ilimchukua muda kunyanyua mkono ili tusalimiane. Kilikuwa kitambo kifupi mno kushuhudia mabadiliko makubwa. Edward ameondoka. Hajaandika tawasifu (autobiography) yake. Hili ni deni zito ambalo familia haina budi kulibeba. Familia ya Edward, kwa niaba ya baba yao, inabidi waandike wasifu ambao utajibu maswali mengi. Mjane wa Lowassa ashindwa kujizuia

Nini kilitokea afya ya Edward ikabadilika ghafla? Sakata la Richmond halikumtikisa kiafya, ndiyo sababu hadi Novemba 2010 alikuwa imara. Kipi kizito kilimtokea Edward kati ya mwaka 2011 na 2012? Familia inaweza kueleza siri hii.

Simulizi za marafiki ni kuwa Edward aliumia kuitwa fisadi, ila ilimnyong’onyesha zaidi kuona hadi watoto walimwita hivyo. Hili neno lilikuwa na athari kubwa kiasi gani kwenye maisha ya Edward?

Edward ameondoka bila kueleza kwa kina upande wake kuhusu Richmond na jinsi yeye binafsi alivyohusishwa. Hotuba yake bungeni Februari 7, 2008, hata maelezo aliyoyatoa nyumbani kwake Dodoma, katika safari yake ya kutia nia kuwa mgombea urais 2015, Edward aliishia kulalamika badala ya kukata mzizi wa fitina.

Richmond ni balaa la nani? Msabaha, Mungu amrehemu, alisema ni dude la Edward na Rostam. Kisha, Edward na Rostam wakakana. Edward alisema ni yeye alipendekeza Richmond wasipewe pesa baada ya kuona ni wababaishaji.

Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, alivumishiwa kuwa Richmond ilikuwa mali yake. Oktoba 24, 2015, Jakaya alijibu makombora kwa kurejesha kashfa ya Richmond kwa Edward. Jakaya alisema, ni yeye alikataa kuidhinisha fedha kuwalipa Richmond.

Jakaya alihoji: “Kama Richmond ingekuwa yangu, si ningeruhusu malipo?” Jakaya alimsema Edward kuwa alikosea kuingilia mchakato wa zabuni ulioipa kazi Richmond. Edward hajawahi kukiri kuingilia mchakato zaidi ya kutimiza wajibu wake kama waziri mkuu.

Richmond ilimalizwa bungeni kwa mtindo wa “funika kombe mwanaharamu apite”. Ungemsikiliza Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alikuwa na ukweli wake. Rostam na Edward wa kwao. Msabaha aliamini tofauti, vivyo hivyo kwa Jakaya. Tanzia ya Lowassa

Tawasifu ya Edward ingeweza kuisogeza nchi kwenye ukweli kuhusu Richmond na matokeo yake. Bahati mbaya ameondoka bila kutimiza wajibu huu muhimu. Familia inatakiwa kuandika wasifu, ieleze hisia za Edward kuhusu Richmond na ukweli alioutamka kwenye meza ya chakula nyumbani. Yapo maneno kuwa Richmond ilitengenezewa ripoti mbili. Moja iliyokuwa haimgusi kabisa Edward na nyingine iliyomning’iniza, ambayo ndiyo ilisomwa na Mwakyembe bungeni. Ukweli ni upi? Kwa nini Richmond imekuwa tamthiliya yenye mwisho tata kuwahi kutokea katika historia ya Bunge la Tanzania?

Hata baada ya sakata la Richmond, Edward alionesha bado alikuwa na uhusiano mzuri na Jakaya, aliposema: “Mimi na Rais Kikwete hatukukutana barabarani.” Naye Jakaya alimpoza Edward, katika hotuba yake ya kufunga Bunge la Tisa, alipomsifu kwa kufanya naye kazi vizuri na kwa mafanikio kabla ya kupata “ajali ya kisiasa”.

Kitabu kidogo cha wasifu wa marehemu, maalumu kwa ajili ya Edward, hakuna popote kulikuwa na picha ya Jakaya. Hata salamu za rambirambi, zimechukuliwa za wengi, lakini hakuna mahala popote kwenye kitabu, kuna jina la Jakaya, neno lake wala picha.

Marafiki ambao hawakukutana barabarani, wakaitwa “Boys II Men”, kwa mtindo wao wa kazi na jinsi walivyofanana na kuchangia rika. Matendo ya wakati wa msiba wa Edward, yamedhihirisha uwepo wa ufa mkubwa kifamilia, kutoka familia ya Edward hadi ya Jakaya.

Matendo hayo yanatoa ujumbe kuwa kutoka kwa Edward hadi familia yake, kuna mengi vifuani kuhusu Jakaya. Edward angeandika kitabu, angalau angeweka wazi hisia zake. Hili ni deni kwa familia. Nini kilikuwemo kwenye kifua cha Edward?

Kihulka, Edward hakuwa mtu wa kurushiana maneno. Inawezekana ni kwa sababu hiyo, hakutaka kuzungumza mengi kuhusu maumivu yake ya kisiasa. Pamoja na hivyo, haiwezekani akose watu wachache aliowaamini aweze kuwasimulia, hususan familia yake.

Kwa mantiki hiyo, familia inayo nafasi ya kuandika kitabu cha Edward na kuelezea kinagaubaga hisia zake za maumivu, kuandamwa, usaliti na jasho alilovuja kumpeleka Jakaya Ikulu, halafu akapigwa kikumbo ndani ya miaka miwili, kisha akabaki mtazamaji.

Kila mmoja anaweza kupata picha inauma kiasi gani kushiriki kuandaa shamba, kulima, kupanda mbegu, kuweka mbolea na kumwagilia maji. Mazao yanastawi. Wakati wa mavuno, jasho lako halithaminiwi tena. Unapigwa kikumbo ukae kando.

Baada ya hapo, unaanza kuwashuhudia watu ambao hawakuwepo nyakati ngumu za kilimo, wakifaidi matunda. Ndivyo unaweza kupata picha jinsi Edward alivyojisikia. Watu wengi waliojipambanua kama maadui wa Edward, walilamba uteuzi kwenye Serikali ya Jakaya, ambayo Edward aliivujia jasho. Rais Samia kushiriki ibada ya mazishi ya Lowassa

Kiini cha mgogoro wa Jakaya na Edward ni nini? Sitta alitajwa kuwachonganisha. Ukweli ni upi? Sitta alifariki dunia Novemba 7, 2016. Hakuacha kitabu. Mwakyembe aliahidi wakati wa msiba kuwa ataandika kitabu cha Sitta. Huu ni mwaka wa nane, hakuna kitabu.

Ilifikia hatua hadi Sitta alitangaza kuwa kuna watu waliweka uchawi bungeni. Edward na Sitta hawapo. Familia za Edward na Sitta, kwa taarifa zao na kuchanganya na zilizopo kwa watu wengine wa karibu, wanaweza kukata kiu.

Edward alikuwa na ndoto ya urais kwa muda mrefu. Mwaka 1995, akiwa na umri wa miaka 42, alijitengeneza na akawa na nguvu, hasa miongoni mwa vijana. Kwa nini aliamua ndoto yake ya urais kuiundia upacha na Jakaya? Alimwamini kiasi gani Jakaya, alipojiweka kando kutogombea urais mwaka 2005, akaamua kuwa “Timu Jakaya?” Kadiri maswali yanapokuwa mengi, ndivyo na madeni ambayo Edward ameiachia familia yake, yanavyoongezeka na kudhihirika. Uhusika wa Edward kwenye siasa za nchi, mengi chanya aliyoyafanya, yalifunikwa na kashfa za ufisadi. Hili lilimtesa kiasi gani?

Edward ni kitabu cha siasa za Tanzania. Familia yake inatakiwa itambue hilo na kulipa madeni ambayo wameachiwa. Historia ya maisha ya Edward, jinsi alivyopigana vita vyake, alivyoshinda na alivyoanguka, taifa linapaswa kusoma. Wanasiasa hasa wa kizazi kipya, wanahitaji kujifunza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live