Arusha. Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwa ujasiri wake na kuilinda na kutetea Katiba huku akitaka taarifa hiyo kufanyiwa kazi ipasavyo.
Akizungumza na Mwananchi leo kuhusiana na taarifa ya CAG ambayo imewasilishwa bungeni leo, Lema amesema kama CAG angekuwa mtu dhaifu angekuwa tayari amejiuzuru kutokana na maazimio ya Bunge.
"Duniani tuna watu wachache sana waadilifu na wenye uwezo kama Profesa Assad, taifa tunapaswa kujivunia na kumuunga mkono na siyo kumkatisha tamaa kutokana na kazi ambazo anafanya kwa maslahi ya taifa hili," amesema.
Lema amesema Profesa Assad amesimamia Katiba na ameonesha hakuna ambaye yupo juu ya Katiba na kwamba ameweza kuendelea na kazi yake kwa uadilifu mkubwa kwa kutoa taarifa ambayo sasa inapaswa kufanyiwa kazi.
"Amesimamia Katiba, hoja na uadilifu, ametoa mapungufu mengi katika matumizi ya Serikali, vyama vya siasa na mashirika ya umma, ingawa kuna mengine hayajawekwa wazi, lakini uwezo wake umejidhihirisha," amesema.
Akizungumzia yaliyogunduliwa na CAG, ikiwapo ununuzi wa gari la Chadema na CCM kutotoa makato ya wafanyakazi, alisema ana amini majibu yatatolewa na kwa upande wa Chadema alisema suala hilo litatolewa ufafanuzi na viongozi wa kitaifa kwani hakuna ubadhirifu.
Related Content
- VIDEO: CAG abaini hasara ya mamilioni Nec
- Serikali Tanzania yachangia Sh7 bilioni kati ya Sh118 bilioni za miradi 10
- Profesa Assad ataja mashirika 14 yenye hali mbaya kifedha
- CAG amuibua tena Lugumi kwenye ripoti yake