Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubenea, Polepole wanavyomzungumzia Mengi

56148 Kubeneapic

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema licha ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi kuonekana  mwanachama wa CCM, hakuwahi kuweka mbele itikadi za vyama, alijali zaidi maendeleo ya watu.

Amesema Mengi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 2019 aliweza kutumia rasilimali zake kusukuma ajenda ya rasilimali za nchi bila kujali nani alibeba ajenda hiyo na alitumia fedha zake kusaidia vyama vyote.

Kubenea ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 7, 2019 wakati wa kuaga mwili wa mfanyabiashara huyo kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

“Jambo muhimu kwake ilikuwa ni ajenda ya nchi na maendeleo ya watu. Milango yake ilikuwa wazi kwa watu wa itikadi zote na alithamini utu wa mtu kuliko itikadi za vyama.

“Kama tunataka kumuenzi kwa dhati ni muhimu kuiga mfano huo, tusijifanye tunampenda sana Mengi wakati tunabaguana. Ilani za vyama vyote katika uchaguzi wa 2015 zilisheheni mawazo ya Mengi,” amesema Kubenea.

Naye Polepole amesema chama chake kinajivunia Mengi kuwa mwanachama wake kwa maelezo kuwa, alikuwa mshauri mkubwa wa masuala ya uchumi na biashara.

Habari zinazohusiana na hii

Polepole amesema mfanyabiashara huyo alikuwa bilionea mjamaa, alihangaika kuhakikisha kila binadamu anakuwa sawa na mwingine bila kujali hali wala nafasi yake na vilevile ndani ya CCM alikuwa kiungo kati ya chama na Serikali na wadau wa sekta binafsi.

“Alikuwa daraja kati ya sekta binafsi, CCM na Serikali yake, kila panapokuwa na mkwamo kabla mambo hayajaharibika Mzee Mengi alisimama kama kiungo kati ya chama, Serikali na wadau wa sekta binafsi ambao chama chetu kinaamini sana kwamba uchumi wetu unategemea ukuaji na uimara wa sekta hiyo,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz