Katika Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa nchini Tanzania - uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaaam wiki hii, mjadala juu ya katiba mpya uliibuka.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia ufunguzi wa mkutano huo amesema: “Kuhusu Katiba Mpya tunaanza na Elimu, Watanzania waijue. Unaanzaje kumwambia mtu akupe maoni yake na kitu hakijui. Viongozi wa kisiasa tunadhani tuna haki ya kuburuza watu, tunachokisema sisi watu wote wafuate, tunageuza watu makasuku.”
Maoni ya Watanzania katika mitandao ya kijami yamegawika makundi mawili, juu ya kauli hii. Wapo wanaoiona ni kauli yenye nia njema, kwa kuzingatia ahadi chanya za muda mrefu za Rais Samia juu ya katiba mpya.
Wengine wakiitazama kama mwendelezo wa ucheleweshwaji wa kupatikana katiba mpya, wakati wananchi tayari walishatoa maoni yao juu ya yale wanayoyataka katika katiba hiyo miaka mingi iliyopita.
Ulipoanza na ulipokwama Wakati wa Kikwete: Mchakato wa Katiba mpya Tanzania ulianza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013. Wakati huo rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akiwa madarakani.
Kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ikaanzishwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikuwa chini Uenyekiti wa Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba.
Tume hii ndiyo iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba.
Rasimu hii ya pili maarufu kama Rasimu ya Warioba ikawasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba (BMK), ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa na wajumbe wengi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi -Zanzibar.
Bunge maalumu la Katiba - Makamu Mweyekiti wake alikua Samia Suluhu Hassan kabla hajawa rais, chini ya Uenyekiti wa marehemu Samuel Sitta (spika wa zamani wa bunge), ndiko kulikoibuka mivutano mikali kuhusu masuala kadhaa hasa lile la idadi ya serikali katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kutokana na mvutano mkali baadhi ya wajumbe hasa kutoka upinzani waliamua kujitoa na kususia mchakato. Waliobaki ambao wengi walikuwa wa chama tawala (CCM) waliendelea na mchakato. Ikapatikana Katiba pendekezwa ambayo ilipaswa kupigiwa kura ya maoni. Mchakato ukaishia hapo 2014, na hakukuwa na kura ya maoni mpaka leo.
Wakati wa Magufuli: Hakuna mambo mengi ya kueleza kuhusu mchakato wa katiba mpya wakati wa utawala wa hayati Rais John Pombe Magufuli. Katika kongamano la Novemba 2018 la kujadili hali ya siasa na uchumi wa nchi lililojumuisha wasomi na viongozi kutoka katika sekta mbalimbali za serikali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema:
"Sitegemei kutenga fedha kwa ajili ya watu kula wakakae bungeni kujadili katiba, hata kama kuna mtu anataka kutupa hizo fedha, atupe tukatengeneze reli. Watu wanakaa wanapiga kelele katiba mpya, utadhani katiba ndio mwarubaini wa kila kitu."
Wakati wa Samia: Ajenda ya katiba mpya inaonekana ipo katika kichwa cha Rais Samia Suluhu Hassan. Hata hutuba ya hivi karibuni katika Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa, kauli zake zinashiria hivyo.
Katika juhudi zake za kulifanikisha hilo aliunda kikosi kazi kilichoongozwa na mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Rwekaza Sympho Mukandala na kuratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa. Miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa na kikosi hicho, ni kuanzishwa tena mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Huku rais Samia akionekana na nia njema juu ya katiba mpya, changamoto ni lini ajenda hiyo itakamilika. Limekuwa ni suala la kuzunguzwa, kisha kimya hutanda, halafu huzungmzwa tena na kimya kingine hufuata.
Katiba mpya inapigwa danadana?
Baada ya vurugu za kisiasa za mwaka 2007–2008, zilizosababisha vifo. Kenya iliona uhitaji wa kuwa na katiba mpya. Na kufikia Agosti 2010 taifa hilo likawa na katiba mpya ambayo inafanya kazi hadi sasa. Ni kipindi cha miaka miwili na miezi kadhaa tu.
Lakini nchini Tanzania ni zaidi ya miaka kumi tangu mchakato wa katiba mpya uanze. Hii ni dalili tosha kwamba viongozi wenye nguvu za kukamilisha mchakato huo - ili hatimaye ipatikane katiba, wanapiga chenga na danadana.
Miaka kumi ni kipindi kirefu mno kwa katiba kuwa bado haijakamiliki. Fauka ya yote, haijulikani itakamilika lini, wala mchakato wenyewe utaanza lini.
Kuna ukweli kwamba mchakato huu unakumbwa na utata juu ya wapi unapaswa kuanza; uanze katika hatua ya kukusanya tena maoni ya wananchi, au uanze kwenye bunge maalumu ama uanze kwa wananchi kupigia kura rasimu ambayo ilisusiwa na vyama vya upinzani!
Yumkini panahitajika uamuzi wa pamoja miongoni mwa wale waliohasimiana 2014, hapa nazungumzia wanasiasa wa upinzani na wale wa chama tawala ili kuufanya mchakato ukubalike pande zote.
Ingawa hilo halipaswi kuwa chanzo cha mchakato ukwame kwa kipindi chote hicho, ikiwa wale wenye mamkala wangekuwa na utashi wa kutaka katiba. Yaonekana upande wa chama tawala hauna haraka na katiba mpya. Bahati mbaya ndio upande wenye mamlaka makubwa ya kuamua kuhusu lini mchakato wenyewe uanze.
Kwa ahadi ya rais Samia juu ya mwendelezo wa katiba mpya. Sanjari na tume ambayo aliiunda ili kutafuta maoni; itakuwa ajabu ikiwa ataondoka madarakani bila kukamilisha kile ambacho anaamini kinapaswa kukamilishwa.