Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigwangalla aweka bayana alichoteta na Fatma Karume

44625 Pic+kigwangala Kigwangalla aweka bayana alichoteta na Fatma Karume

Mon, 4 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema ni muhimu kwa walio serikalini kujenga utamaduni wa kusikiliza mawazo ya wale wanaowapinga kwa kuwa siku zote kusikiliza huja na kitu kipya cha kujifunza.

Waziri Kigwangalla amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati akijibu swali la Mwananchi kuhusu mazungumzo yake na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, ambaye ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Serikali na viongozi wake.

Wawili hao walikutana Januari 13 jijini Dar es Salaam kisha picha walizopiga wakiwa pamoja zikazua mijadala na maswali lukuki kutoka kwa watu mbalimbali.

Lakini Waziri Kigwangalla haoni kama kuna tatizo kukutana na mwanaharakati huyo wa haki.

“Sikuwahi kukutana naye wala kuwahi kusalimiana naye. Ile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana naye,” alisema Kigwangalla.

“Nilitamani kumsikiliza ili niweze kujifunza kwa nini anafanya (vitu) anavyofanya.”

Alisema alikuwa anaamini Fatma, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, asingeweza kuwa mkosoaji wa Serikali kutokana na familia yao kuishi Ikulu.

Mbunge huyo wa Nzega Vijijini alisema mara baada ya kukutana na Fatma na kuzungumza naye, amebaini ni mtu mzuri na anayeelewa zaidi na kwamba anachokifanya ni sahihi.

Alisema kutokana na ukweli kwamba Fatma ni mwanaharakati, hawezi kunyamaza anapoona mambo hayaendi sawa.

Waziri huyo alisema mazungumzo yake na Fatma yaliyochukua zaidi ya saa tano, yalimpa fursa ya kumjua vizuri Fatma na sababu za mambo anayofanya.

“Fatma hana nia mbaya, anachokifanya ni kusema tu na kwa mujibu wa Katiba yetu ni haki yake kufanya hivyo,” alisema.

“Nikagundua kuwa ni mtu mwenye busara sana na uelewa mpana tu wa mambo kadhaa. Fatma hana shida yoyote ya kibinafsi na Rais (John) Magufuli au Serikali yake kwa ujumla.

“Mkikaa pamoja hamuwezi kushindana, kuna mambo mtakubaliana na kuna mengine mtaeleweshana.

“Kwa hiyo inasaidia sana kubadili mitazamo ya watu kwa kiasi kikubwa tu na inawezekana na yeye (Fatma) kabadili mitazamo fulani.”



Chanzo: mwananchi.co.tz