Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema huwezi kuiandika historia ya waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ukaliacha neno Chadema.
Amesema hayo akitoa salamu baada ya maziko ya Lowassa yaliyofanyika Leo Februari 17, 2024 kijijini Ngarash wilayani Monduli mkoani Arusha.
“Rais nashindwa kujua vizuri nizungumze nini kuhusu Lowassa lakini niombe kwa sababu ya rekodi niweke kumbukumbu sahihi.
“Huwezi kuiandika historia ya Lowassa ukaliacha neno Chadema, huwezi ni kujidanganya tu na kujaribu kuiua historia ambayo huwezi kuiua,” amesema Mbowe. Kauli ya Mbowe akitoa salamu maziko ya Lowassa
Rais Samia Suluhu Hassan amewaongoza maelfu ya waombolezaji katika maziko hayo.
Mbowe amesema amesikiliza na kusoma historia ya Lowassa kama ilivyowasilishwa na kuongeza:
“Binafsi ni mtu mkweli na nimesikitika kwa sababu kwa kweli amefanya mambo makubwa ndani ya Serikali, ndani ya CCM na vyama vya upinzani na katika Taifa letu na Taifa hili ni letu sote.”
“Unawezaje kuandika historia ya Lowassa ukasahau utumishi wake wa miaka minne kama mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, mgombea urais wa mwaka 2015 ambaye alijenga demokrasia kwa viwango ambavyo haijawahi kufikiwa na mgombea yeyote wa upinzani katika Taifa letu hili,” amesema Mbowe.
Amesema, “Nilisema niliseme hili kwa sababu Taifa letu hili ni letu sote na viongozi wengine wote wakuu wapo hapa, Lowassa alikuwa mtu wa karama tumesikia sifa zake nyingi tangu siku ya kwanza hadi siku ya leo ya tamati.”
Amesema kipekee anatambua alikuwa mtu wa karama ya ajabu aliyeweza kuunganisha makundi mbalimbali kwa wakati wote, na alikuwa na unyenyekevu mkubwa.
“Wenzangu mtatambua kuwa Lowassa alianza safari ya matumani ndani ya CCM baada ya hapo hayo mimi siyazungumzi, baadaye akahamia safari ya mabadiliko ndani ya Chadema, huyu ni mtu alileta kasi ya ukuaji wa demokrasia ndani ya nchi yetu,” amesema Mbowe.
Amesema alilifanya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na wabunge 115 kutoka vyama vinne vya upinzani.
“Hili ni jambo linalopaswa kuzungumzwa kwa sababu ni hatua ya ujenzi wa demokrasia katika Taifa letu,” amesema.
“Huyu ni kiongozi aliongoza uchaguzi na kuwezesha madiwani zaidi ya 2,000 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania karibu nusu ya madiwani wa nchi yetu.”
Vyama vingine tofauti na CCM vikaongoza Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Moshi, Mtwara, Iringa na Mbeya hampaswi kupuuza historia hii viongozi wangu, tunatakiwa wakati wote tumuenzi Lowassa kwa sababu ni katika ujenzi wa demokrasia na ujenzi wa Taifa letu sote,” amesema.
Amesema Lowassa ni muathirika wa mifumo ya uchaguzi, lakini alikuwa mgombea wa upinzani kupata kura zaidi ya milioni sita haikuwa jambo dogo ni kwa sababu ya karama yake.