Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amekutwa na Korona, taarifa imetolewa na Ikulu ya Marekani.
Makamu huyo wa Rais alikamilisha dozi zote mbili za Uviko-19 akitumia chanjo aina ya Moderna Covid-19 ambayo aliipata kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwezi wa kumi na dozi ya pili alipata Aprili 1.
Makamu huyo wa Rais amepata maabukizi ya Uviko ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu Serikali ya Marekani ilipopunguza vikwazo dhidi ya maambukizi ya virusi vya Uviko- 19.
Kwa mujibu wa sheria za Afya ya Jamii wageni wote na maafisa hawaruhusiwi tena kuvaa barakoa au kujitenga katika shughuli mbalimbali katika Ikulu ya Marekani White House.
Taarifa za maambukizi ya Uviko-19 jijini Washington Marekani zimepungua kwa asilimia kubwa tangu zilipotikisa zaidi mapema mwezi Januari ambapo Serikali ilikabiriana na kesi nyingi za maambukizi hayo.
Licha ya kwamba Ikulu ya Marekani White House imekuwa ikiendelea kufanya shughuli zenye kuhitaji watu wengi uvaaji wa barakoa umekuwa ni hiari na maafisa wengi kutoka White House wamesahau kabisa suala zima la kuvaa barakoa mbele ya hadhara.
Kumekuwa na sheria ya lazima kupimwa kwa wale wanaokutana moja kwa moja na Rais Joe Biden na wanalazimika pia kukaa naye mbali katika vikao na mikutano mbalimbali.
Katibu wa Habari wa Ikulu ya Marekani White House, Jen Psaki amedai kuwa Ikulu hiyo haina mpango wa kurudi enzi za kuweka vikwazo juu ya tahadhari za kujikinga na maambukizi ya Uviko-19.
"Tunaendelea kutekeleza sera ya watu kurudi kuwajibika makazini na tunahisi kuwa tuna sababu za kufanya hivyo,” alisema Psaki.