Dar es Salaam. Familia ya Dewji imetangaza dau la Sh1 bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa bilionea Mohamed Dewji, hatua inayoonyesha kuongezeka kwa ugumu katika sakata hilo.
Wakati familia ikisema hayo, kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliliambia Shirika la Habari la Ujerumani jana kuwa kuna dalili kwamba watekaji wamefanya hivyo kwa lengo la kushinikiza wapewe fedha na si watu wanaotaka kulipiza kisasi.
Dau lililotolewa jana ni kubwa kuliko lolote lililowahi kutolewa na familia inayomtafuta ndugu aliyetekwa au kupotea, au iliyowahi kutolewa na Jeshi la Polisi wakati ikimsaka mhalifu nchini.
Mfanyabiashara huyo tajiri na kijana alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi saa 11:30 alfajiri wakati akiwa Hoteli ya Colosseum na hadi jana hakuna taarifa zozote za watekaji, lengo la kumteka wala fununu za alikohifadhiwa, ingawa polisi inashikilia watu 26 kwa ajili ya kuwahoji.
Kabla ya kukutana na waandishi wa habari, familia hiyo ilikuwa kimya tangu alipotekwa, wakati Mtaa wa Laibon uliopo Oysterbay anakoishi mfanyabiashara huyo tajiri barani Afrika, una ulinzi unaohusisha ukaguzi wa magari yanayopita.
Mkutano wa jana ulioanza saa 7:00 mchana katika ofisi zake zilizopo jengo la Golden Jubilee jijini Dar es Salaam ulifurika waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali na wengine walikataliwa kuingia kutokana na kujaa kwa ukumbi.
Gulam Hussein, baba wa mfanyabiashara huyo na muasisi wa kampuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL), aliingia ukumbini akiwa ameongozana na Azim Dewji, mfanyabiashara maarufu na mfadhili mkuu wa zamani wa Simba, meneja miradi wa kampuni hiyo, Soud Mwanasala na dereva wa Mo Dewji.
Azim, aliyejitambulisha kama msemaji wa familia hiyo, ndiye aliyejongea vinasa sauti kwa ajili ya kusoma taarifa ya familia iliyokuwa na dau hilo.
“Familia ya Bwana na Bibi Gulam inasikitika kutekwa kwa mtoto wao mpendwa saa 11:35 alfajiri mpaka saa 11:40 alfajiri. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, serikali, taasisi zake kwa jitihada kubwa za kuhakikisha mtoto wetu anapatikana,” Azim alisoma taarifa hiyo.
“Katika kuongeza juhudi za kuhakikisha mtoto wetu anapatikana mapema, familia tunatangaza zawadi nono ya Sh1 bilioni kwa yeyote atakayefanikisha taarifa za kupatikana kwa Mo Dewji.”
Azim alisema familia itatunza siri za mtoaji wa taarifa atakayesaidia kupatikana kwa Mo Dewji, ambaye ameshinda zabuni ya kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya michezo ya Simba.
Azim, Gulam na Mwanasala, hawakukaribisha maswali na wakati wote mzazi huyo wa Mo Dewji, anayeonekana kuwa na umri wa kuanzia miaka 70 na aliyevalia shati jeupe na suruali ya rangi ya khaki, alionekana kutawaliwa na fikra.
Alikuwa katika hali ya unyonge na muda mwingi alikuwa akiinamisha kichwa, huku akishika shavu mara kadhaa.
Waandishi wa habari walianza kuingia ukumbini saa moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo na hadi ulipokaribia kuanza walifikia takriban 100 ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosabisha baadhi kuzuiwa kuingia.
Hata waliokuwa ndani walipunguzwa na waratibu wa mkutanao huo ambao walitaka kila chombo kiwakilishwe na mwandishi mmoja.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa amesema huenda watu waliomteka Mo Dewji wanataka wapewe kiasi fulani cha fedha, kwa mujibu wa tathmini yake.
Alisema kama watekaji walikuwa watu wa kulipiza kisasi, wangeweza kumuua kwa sababu walifyatua risasi mbili kabla ya kuondoka naye hotelini, silaha ambazo wangeweza kuzitumia kumuua kama wangekuwa walipizaji kisasi.
Mambosasa aliiambia Deutche Welle jana kuwa ingawa watekaji hawajasema wanataka nini, lakini dalili zinaonyesha ni watu wa aina hiyo.
Alisema hadi jana, Jeshi la Polisi linawashikilia watu hao 26, ambao wengi wao ni wafanyakazi wa hoteli na walinzi. Alisema walinzi wanashikiliwa kwa sababu ya hali ya uzembe ulioonekana siku ya tukio, wakati wafanyakazi wengine wanashikiliwa kwa sababu picha za kamera za CCTV hazionyesha vizuri tukio hilo.
Mo Dewji, ambaye alifanikiwa kukuza kampuni ya baba yake kutoka mapato ya dola 30 milioni za Kimarekani hadi dola 1.5 bilioni kati ya mwaka 1999 na 2018, ni mtoto wa pili kati ya sita wa familia ya Gulam na Zubeda Dewji.
Ni msomi aliyesomea biashara ya kimataifa na fedha nchini Marekani na kampuni yake ambayo imetapakaa katika nchi 11 za barani Afrika, imeajiri zaidi ya wafanyakazi 24,000.