Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

IGP Sirro: Tunamsubiri kwa hamu Tundu Lissu

48498 Pic+lissu IGP Sirro: Tunamsubiri kwa hamu Tundu Lissu

Wed, 24 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi nchini, limesema linamsubiri kwa hamu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ili limhoji kupata ushahidi wa tukio la kushambuliwa kwake.

Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 cha ITV juzi usiku, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, alisema tangu awali, tukio la kushambuliwa Lissu lilikosa ushirikiano wa ushahidi.

“Suala la Lissu ushirikiano ulikuwa hakuna kabisa na lilichangia upelelezi wetu kuwa mgumu. Hata dereva wake tulipokwenda kumhoji, hakutaka kuonyesha ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

"Wewe umeshuhudia tukio, halafu polisi wamekuja kukuhoji, hutaki hata kuwapa fursa ya kutaka wakuone, hapo sasa unategemea polisi watafanya nini?" alihoji.

IGP Sirro alisema hata kama Lissu akiishi Ulaya na kurudi Tanzania baada ya miaka 20, lazima Jeshi la Polisi litamhoji tu kuhusu tukio la kushambuliwa kwake.

“Sasa ninashukuru kwamba kwa vile anagombea urais, na kama atapewa nafasi na chama chake, ninafikiri atakuja nchini na tutamhoji vizuri tupate maelezo yake kwa sababu upelelezi au tukio huwa halifiki mahala likawa mwisho.

"Hata kama angekaa Ulaya miaka 20, akija bado tutamhoji kujua ukweli wa jambo. Lakini kwa vile anakuja, niombe aje, maana yake nina haja sana ya kutaka kuja kumhoji, ili kujua ukweli wa jambo lenyewe likoje," alisema.

IGP Sirro alisema upelelezi ni suala mtambuko na kwamba wakati mwingine umekuwa ukichelewa zaidi kwa sababu lazima ushirikishe mamlaka nyingine.

“Sula la upelelezi ni mtambuka, kwa sababu mfano mtu amekufa, ni lazima ushirikishe Mkemia Mkuu wa Serikali, madaktari, kwenye tukio umeona kitu gani?

"Kwa hiyo, siyo suala la mara moja unapata majibu au ushahidi wa kuthibitisha kosa. Wakati mwingine inategemea na ugumu wa tukio lenyewe,” alifafanua.

Alikiri kuwapo kwa baadhi ya matukio ambayo ushahidi wa kutosha umekuwa ukikosekana na yamekuwa yakiondolewa kwenye uchunguzi wao, lakini kwa matukio makubwa, likiwamo la Lissu, si rahisi kuyaondoa.

“Kwa mfano suala la Tundu Lissu bado hatujapata maelezo yake, tunalifungaje hilo jalada? Ni lazima tumsubiri tupate maelezo yake ili tuone kama kuna vitu anaweza kutusaidia kupata majibu ya malalamiko yake,” alisema.

Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risali katika sehemu mbalimbali ya mwili wake Septemba 7, 2017 mchana alipokuwa anajiandaa kushuka kwenye gari nyumbani kwake jijini Dodoma muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Bunge, ambacho pia alishiriki kuchangia hoja.

MBOWE KUSHTAKIWA?

Akizungumzia madai ya kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, IGP Sirro alisema bado uchunguzi wake unaendelea na kwamba endapo watabaini kwamba taarifa zilizotolewa ni za uongo, watampeleka mahakamani.

“Suala la Mbowe tunaendelea kuchunguza, nilitoa maelekezo tupate ushahidi maana ushahidi namba moja siku zote ni kwenye eneo la tukio. Sasa kama eneo la tukio ushahidi hakuna na kila mtu anasema hajasikia... hajasikia…. hajasikia! Sitaki nimhukumu mtu, lakini upelelezi unaendelea.

"Ila ninataka Watanzania waelewe kwamba tukibaini kuna taarifa ya uongo, ninarudia... tukibaini kuna tarifa ya uongo, hakuna mtu aliye juu ya sheria, tutampeleka mahakamani kwa kutoa taarifa ya uongo," alisisitiza.

IGP Sirro pia alikiri Jeshi la Polisi kulazimika kutumia nguvu ya ziada kumhoji dereva wa Mbowe, akifafanua: "Kwa mfano, wakati tunajaribu kumhoji dereva wake, alizuiwa asiseme chochote na ilibidi tutumie nguvu ili aseme chochote. Kwa mazingira hayo, inakuwa na mashaka makubwa sana."

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi aliongeza: "Mtu anaposhambuliwa ni lazima tupeleleze, ili tujue -- je, ni kweli kashambuliwa? Kwa sababu si kila taarifa huwa ni sahihi."

Mbowe alidaiwa kushambuliwa Juni 8, mwaka huu na watu wasiojulikana nyumbani kwake jijini Dodoma na kulazimika kukimbizwa katika kituo cha afya jijini huko kisha kuhamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

UCHAGUZI MKUU

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, IGP Sirro alisema wamejipanga kuhakikisha unafanyika katika hali ya amani na usalama na hawatamvumilia mwanasiasa yeyote atakayejaribu kuchochea vurugu.

“Kuelekea Uchaguzi Mkuu, tumejipanga vizuri, hata kama ungefanyika leo. Sisi wenyewe ndani tunapeana elimu kwa sababu unaposimamia kanuni au sheria ni lazima uzijue.

"Wakati wa uchaguzi kuna kanuni na taratibu zake, sasa wakati wa uchaguzi lazima kila kinachofanyika kiwe ni halali na kama si halali ni kuvunja sheria na huwezi kuachwa.

"Kama ni maandamano, kuna utaratibu wake na lazima ufuatwe na kama hujafuata utaratibu, unakuwa umevunja sheria na umekuwa mhalifu," alifafanua.

Alitahadharisha makundi ya watu ambao hufanya vurugu katika vituo vya kupigia kura kwa madai ya kulinda kura, akisisitiza kuwa hawatawavumilia.

"Hayo mamlaka ya kulinda kura wameyapata wapi? Na kama hakuna kanuni ambayo imetoa mamlaka ya kulinda kura, maana yake unavunja sheria na ukivunja sheria, tutakushughulikia kwa mujibu wa sheria ile ambayo umeivunja wewe.

"Niwaambie Watanzania kwamba taratibu zipo, mahakama zipo, ukiona hujaridhika, utaenda mahakamani, lakini suala la kuamua kuvunja sheria, ninasikitika sana kwamba mwishowe utajialaumu kwa sababu utakuwa umetaka mwenyewe.

"Nilisikia kiongozi mmoja anasema damu itamwagika, mimi nilisikitika sana, unataka kuwa kiongozi, lakini unataka watu wamwage damu. Imwagike ya Watanzania au imwagike ya kwako?

"Kabla hujasema jambo, unatakiwa ulifikirie mara mbili kwamba unasema hayo kwa faida ya nani? Je, hiyo damu inamwagika, serikali ipo au haipo?

“Kama serikali ipo, maana yake suala la damu kumwagika halipo na kwa bahati nzuri Watanzania wengi hawapendi kumwaga damu kwa sababu ya uchaguzi.

"Niwaombe sana hii mihemko mingine haina tija, kama kuna jambo halijaenda vizuri, wafuate taratibu, wasijiingize kwenye uhalifu kwa sababu tutakumbana tu.

“Mimi nipo, vyombo vipo, jeshi lipo, hatutakuacha, yaani kwa sababu ya 'interest' (maslahi) yako wewe mtu mmoja, ufanye watu wafe?" alionya.

IGP Sirro pia alizungumzia kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na hadhara, akisema kufanyika kwake kuna taratibu zake ambazo lazima zifuatwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live