Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huyu ndiye Reginald Mengi

55296 Mengi+pic

Fri, 3 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanzania imepoteza mmoja wa watu muhimu aliyeacha athari katika maisha ya wengi.

Tajiri maarufu, Reginald Mengi aliyefariki usiku wa kuamkia jana huko Dubai ameondoka akiwa amecha si urithi wa mali tu, bali pia kitabu ambacho pamoja na mambo mengineyo, anaelezea safari yake ya maisha ya dhiki akiwa mtoto hadi kuwa msomi mkubwa fani ya uhasibu na kisha tajiri wa kupigiwa mfano.

Tofauti na matajiri wengine, viongozi na hata watu maarufu wasiopenda kuanika safari za maisha yao, Mengi amefariki akiwa ameacha wasifu wa maisha yake katika maandishi.

Kitabu hicho kilichozinduliwa Julai 2018 na Rais John Magufuli kina utajiri wa hekima, mitazamo, ushauri, wosia kwa watu wa kila kada nchini. Tunapoomboleza kifo chake, ni busara kufanya marejo ya kitabu chake kinachoelezea undani wa maisha yake tangu utotoni.

Mengi ameandika wasifu huo aliouita kwa jina la ‘I Can, I Must, I Will, The spirit of success,’ (Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanya), akielezea maisha yake ya kutoka kuishi katika vibanda vya udongo na kutembea peku kwenda shuleni, hadi kuwa mmoja wa wahasibu wa kiwango cha juu nchini na tajiri wa kupigiwa mfano.

Familia na maisha utotoni

Kitabu anakianza kwa simulizi akiwa mtoto na kuelezea maisha ya ‘kila siku afadhali ya jana’ waliyokuwa wakiishi wazazi wake katika vibanda vya udongo katika Kijiji cha Nkuu kilichopo Machame mkoani Kilimanjaro.

Akiwa mtoto wa tano kati ya saba wa mzee Abraham Mengi na mkewe Ndeekyo, Mengi anasimulia:

“Familia yetu ilikuwa maskini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umaskini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe wachache na kuku.

Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma, ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile.

Mengi na ujasiriamali

Katika kitabu hicho, Mengi anamwita mama yake kwa jina la ‘Nkambusha’ neno la Kichaga linalomaanisha mwanamke mfanyabiashara.

Kumbe ujasiriamali ameurithi na sio tu kutoka mama yake, lakini pia kwa baba yake na kaka yake mkubwa Elitira ambaye Mengi anasema alimvutia mno kwa namna alivyokuwa na sifa za kijasiriamali tangu utotoni.

Moja ya sifa za Elitira ni kugundua fursa na kuzigeuza kuwa miradi ya biashara. Cha kuvutia zaidi, sifa hiyo alikuwa nayo tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi alipoanzisha biashara ya kuuza mayai. Sifa hii ya kaka yake ndiyo ambayo Mengi alikuja kuishi nayo miaka michache baadaye alipoanza kujenga himaya ya biashara.

Mengi aliuvaa ujasirimali nao ukamvaa angali kijana kabisa. Hata hivyo, mifumo ya kiuchumi ya miaka ya 1970, aliiona kama kikwazo kwa ukuaji wa ari ya ujasiriamali kwa Watanzania.

Anatoa mfano wa ‘Operesheni Maduka’ mwaka 1972, ambayo ilishuhudia utaifishaji hata wa biashara ndogo kama mabucha.

“Nilihisi ule moyo wa watu kujihusisha na biashara binafsi na ujasiriamali ukipotezwa na sera na hatua za kiutawala. Nilishangaa uchumi wa nchi ungewezaje kujengwa bila ya kuwa na watu wenye nguvu ya kiujasiriamali,” anaeleza.

Kuanza biashara

Hata, hivyo, mfumo huo haukumkatisha tamaa, aliamini kuwa kwenye matatizo kulalamika pekee hakusaidii, bali mjasiriamali makini ni yule anayetumia hali hiyo kama fursa, si tu ya kibishara, lakini pia kusaidia jamii yake.

Hiki ndicho alichokifanya baada ya kugundua kuwapo kwa uhaba wa kalamu za wino ambazo miaka ya 1983 ilikuwa ni bidhaa iliyoagizwa kutoka nje.

Huo ukawa mwanzo wa Mengi kuingia katika ulimwengu wa biashara akianza na utengenezaji wa kalamu alizozipa jina la ‘Epica kupitia kampuni yake ya kwanza aliyoiita Tanzania Kalamu Co. Limited.

Mradi huo wa kwanza anaosema kwake ulikuwa kama kujaribu kina cha maji katika bahari ya ujasiriamali, aliuanza akiwa hana kitu mfukoni.

Aliagiza vifaa vya kalamu kutoka Mombasa, Kenya kwa mtindo wa mali kauli.

Mpaka anafariki, alishajijengea himaya kubwa ya biashara kuanzia katika uendeshaji wa vyombo vya habari, viwanda vya vinywaji hadi kwenye sekta za madini, gesi, mafuta, kilimo na dawa.

Himaya hiyo aliiongoza kupitia kampuni za IPP Limited jina alilosema lilitokana na kirefu cha Industrial Projects Promotion.

Mtazamo kuhusu uchumi

Mengi amegusa na hata kukosoa mifumo yetu ya kuendesha mambo, hususan upande wa uchumi.

Kwa kiasi kikubwa anachambua mifumo na sera za kiuchumi tangu enzi za Ujamaa mpaka sasa akionyesha nguvu na udhaifu katika maendeleo ya taifa letu.

Kwa mfano, pamoja na Azimio la Arusha kutumika kama chachu ya ujenzi wa mfumo wa kijamii na kiuchumi kwa Taifa tangu mwaka 1967, analishukia kuwa halikuwapa Watanzania fursa ya kushiriki katika maendeleo yao hasa ya kiuchumi.

“Watanzania hawakuweza kufanikisha mawazo na shauku zao za maendeleo ya kijamii na kiuchumi; iliwalazimu kuchagua kutoka katika kile ambacho Serikali iliagiza, anasema”

Unapomsoma, hukosi kubaini kuwa Mengi alikuwa muumini mzuri wa mfumo wa uchumi wa soko. Anaushangaa uongozi wa siasa nchini kuendelea kuushikilia mtazamo wa kijamaa hata katika kipindi ambacho mfumo wa uchumi wa soko ndio unaotamalaki.

Anaamini kuwa katika uendeshaji wa uchumi wa nchi, Serikali inapaswa kuwa kama kocha badala ya kujipa nafasi ya ukapteni wa timu.

Uwekezaji na hatima ya wazawa

Isingetarajiwa Mengi aandike kitabu pasipo kuzungumzia ushirikishwaji wa wazawa katika uwekezaji nchini. Ni kilio chake cha muda mrefu akipinga sera za kiuchumi kuthamini zaidi wageni kuliko wazawa.

Kwa mfano, alitaka kufanyike mabadiliko katika Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Anaandika:

“Kwa umuhimu kabisa, sheria ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, inahitaji kupitiwa na kubadilishwa, ili irandane na mazingira yaliyobadilika ya kiuchumi katika muongo uliopita ambao umeshuhudia wimbi la uwekezaji wa kigeni, huku ukiweka kando masilahi ya wazawa. Haja ya kuwa na uwekezaji wa ndani ni haja iliyo bayana.”

Mengi kama mkosoaji

Mengi, aliamini katika misimamo yake na ndio maana hakuona tabu kukosoa sera na baadhi ya mambo aliyoona yanakwenda ndivyo sivyo nchini.

Pamoja na ukosoaji wake kumjengea uadui na baadhi ya watendaji serikalini, alisema ataendelea kuiwajibisha Serikali, kwa sababu aliamini anayoyakosoa ni kwa manufaa ya mustakabali, amani na umoja wa nchi.

“Natarajia wafanyabiashara wenzangu, wataamka na kutetea misimamo yao, alimradi wanafanya hivyo kwa masilahi ya jamii.”

Alipenda kwao

Akiwa mzaliwa wa kijijini tena mahala alipoishi kwa shida, ingetarajiwa Mengi angekipa mgongo kijiji chake kama wafanyavyo wengi wanaobahatika kupata elimu au ajira.

Kama kijana msomi aliyeiva barabara katika fani adimu ya uhasibu aliyoisomea nchini Scotland, Mengi hakutaka kulowea ‘majuu’ na kufanya kazi huko japo angeweza kufanya hivyo kama ilivyokuwa kwa wasomi wengi wa Kiafrika.

Shauku ya kurudi nyumbani ikamvaa, hata alipopangiwa kazi jijini Nairobi na kampuni ya Coopers Brothers aliyokuwa ameajiriwa, aliomba haraka uhamisho ili akafanye kazi kwao mjini Moshi kwenye asili yake.

Mengi amefariki akiwa na deni moja kwa Watanzania. Ni deni analohitimishia kitabu chake kwamba falsafa yake ya Naweza na Nitaweza, itamsukuma kuendeleza ujenzi wa utamaduni wa ujasiriamali kwa Watanzania wote.

Kwa baadhi inawezekana na alifanikiwa, deni aliloondoka nalo ni kuona Watanzania wote wakifanikiwa.

Huyo ndiye Reginald Abraham Mengi.



Chanzo: mwananchi.co.tz