Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hoja ya utekaji yaibuka tena bungeni, Spika Tulia na Waziri Mkuu watoa maelezo

Tulia Ackson Dp Hoja ya utekaji yaibuka tena bungeni, Spika Tulia na Waziri Mkuu watoa maelezo

Thu, 29 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hoja ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu ikiwemo watoto imeibuka tena bungeni baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest kutaka mkakati wa Serikali kukomesha matukio hayo aliyodai baadhi yanahusishwa na vyombo vya dola.

Leo Alhamisi, Agosti 29, 2024, hoja hiyo imeibuka bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, baada ya Anatropia kusema matukio ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu yanaashiria uvunjifu wa haki za binadamu.

Amesema matukio hayo yamekuwa na sura tofauti tofauti ikiwemo wivu wa mapenzi na ushirikina.

“Lakini na matukio mengine ya kutekwa na kupotea kwa watu yanahusishwa na vyombo vya dola. Nataka kufahamu mkakati wa Serikali kuzuia matendo haya lakini kuondoa taharuki ambayo inajitokeza katika jamii,” amesema.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kabla ya kumpa nafasi Majaliwa kulijibu swali hilo, amesema juzi Jumanne Agosti 27, 2024 alisimama Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani akazungumzia suala hilo.

Amesema mambo hayo yanayohitaji uchunguzi:“Leo asubuhi nimesoma kuna mganga amezika watu sijui 10 na ngapi, sasa huyu mganga ni polisi ambaye watu ameuawa na wamezikwa kwake.”

Amesema mambo hayo yakiwa yanasemwa kwa hisia hivyo inakuwa kama mtu hajali wakati kila mtu anajali na kila binadamu ana haki ya kuishi.

“Lakini tusiweke mazingira kwamba kila anayepotea…si kuna mabasi wanapanda kule chini, akidondoka huko chini si nyumbani wanamtafuta utasema ni chombo cha dola kimemchukua.Sisi lazima tuifanye hii kazi kama viongozi ukichukua mihemko hutoi nafasi kwa Serikali kufanya kazi yake wakati huo huo hutoi nafasi kwa jamii kuendelea kushiriki katika jambo,” amesema.

Amesema wao wote ni viongozi na wangependa wananchi wao wawe salama na kuonya mambo hayo yasichukuliwe jumla jumla.

“Na wewe chukua nafasi ya uongozi, unaweza kutoa ushauri lakini usinyooshe vidole kwa sababu huna hakika. Na wengine wanahama nchi si tunakamata hapa kila siku, na wenyewe huko kwao wanatafutwa watasema chombo cha dola kimewachukua kimewapeleka sijui wapi,” amesema.

Amesema huku kwao wanawatafuta wahamiaji hao waliokamatwa nchini lakini kumbe alipofika hapa Tanzania mazingira yamekuwa magumu na hivyo amekamatwa.

Baada ya maelezo hayo ya Spika Tulia, amempa nafasi Waziri Mkuu Majaliwa kueleza akisema jukumu la kulinda nchi ni wajibu wa Watanzania wote kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama vyenye jukumu la kupokea taarifa mbalimbali zinazoonyesha uvunjifu wa amani popote pale kwenye meza ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Jukumu lao baada ya kupokea taarifa ni kuhakikisha wanafanya uchunguzi,” amesema.

Majaliwa amesema uchunguzi unapobaini waliotenda makosa, wanawapeleka katika vyombo vya sheria.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kujikita kusimamia misingi ya amani katika nchi yetu na usalama kwa kuhakikisha raia na mali zao zinabaki salama.

Amewahakikishia Watanzania kwamba suala la ulinzi na usalama bado liko mikononi mwao pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

“Jukumu letu ni kuhakikisha tunasaidia vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa zozote zile ambazo zinaleta tishio la amani ili kuvisaidia vyombo vyetu viweze kuchukua tahadhari na hatua stahiki ili kubaini watu wote wanaotishia kutokuwepo kwa amani katika nchi yetu,” amesema.

Majaliwa amesema lakini pia vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na wajibu wao wa kuhakikisha kila taarifa inayopatikana lazima ifanyiwe uchunguzi na kubaini wale wote wanaohusika na kama wanapatikana wachukuliwe hatua mara moja.

Amemshukuru Spika kwa maelezo yake ya awali ili kuondoa upotoshaji ambao unaweza kuwa unaendelea na kufanya vyombo vyao vishindwe kufanya kazi yake na kuwavunja moyo watu wanaofanya kazi saa 24 kwa ajili ya ulinzi ambao unawafanya wabaki salama.

MaRC na DC tena bungeni

Katika swali jingine, Mbunge Viti Maalumu, Stella Fiyao amesema nchi inaamini katika uongozi wa kisheria na utawala bora ili kujengwa umoja mshikamano na upendo baina ya wananchi na viongozi wao.

Amesema hata hivyo kumekuwa na changamoto kubwa baina ya baadhi ya wateule wa Rais, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kwa kutumia nguvu na mamlaka yao vibaya kukamata viongozi na wananchi na kisha kuwatupa ndani.

“Moja jambo hili limetengeneza chuki kubwa baina ya wananchi na Serikali yao lakini linafifisha jitihada kubwa za mheshimiwa Rais za kuhubiri 4R na mwisho wa siku jambo hili linakuwa halileti mantiki,” amesema.

Ametaka kujua kauli ya Serikali ni ipi katika kukemea jambo hilo ambalo linatengeneza chuki kubwa baina ya Watanzania na Serikali yao.

“Kauli ya Serikali ni ipi kwa hawa viongozi wanaotumia mamlaka yao kutesa na kunyanyasa wananchi,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema swali hilo ni linafanana na alilolisema jana Jumatano Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi ambapo Dk Tulia aliwapa kazi Serikali kulifanyia kazi.

Amesema wakikamilisha watatoa majibu kwa wabunge hao wawili.

“Lakini kwa utangulizi ni kweli baadhi ya watawala katika maeneo yao wanazo sheria ambazo zinawaruhusu kuhakikisha hali ya utulivu, ulinzi na usalama katika maeneo yao inaimarika,” amesema.

Amesema jambo hilo limeshazungumzwa mara kadhaa bungeni na kutoa ufafanuzi na kuwa wiki mbili zilizopita wakuu wa mikoa na wilaya wote waliitwa katika semina.

“Eneo hili la sheria hili limezungumzwa sana na wameelimishwa sana na tunaamini sasa wamekuwa wanaelewa namna ya kuitumia sheria ile bila kuleta madhara, bila kuleta chuki miongoni mwao baina ya wananchi, bila kuleta mtafaruku katika jamii ili waweze kufanya kazi yao vizuri,” amesema.

Amesema hata kama wanatumia sheria hiyo ni kwa saa 24 ambayo baada ya saa hizo anatakiwa kutoa taarifa kwanini mtu amewekwa ndani, hivyo kuwezesha chombo husika kuchukua hatua.

Amesema baada ya muda huo kama hakuna jambo lolote basi yule aliyewekwa ndani anatakiwa kuachiwa.

Majaliwa amesema wamefuatilia wilayani Kilombero na kubaini watu wote waliokamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero wamepelekwa mahakamani.

“Kwa hiyo jambo lile hatuwezi kulizungumzia tena kwa sababu hatua zilishachukuliwa na watu wale wako mahakamani,” amesema.

Amesema wataendelea kuwaelimisha wateule wote wenye sheria hizi ili waweze kuzitumia kwa weledi, kwa uaminifu na uadilifu, kuzingatia sheria na taratibu za nchi ili kuleta amani jamii bila kuleta migongano isiyokuwa muhimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live