RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kusimulia mahusiano yake na Tanzania, huku akitoa siri iliyomfanya ajenge shule tatu za msingi nchini.
Kadhalika, ametoa siri kwamba asilimia 68 ya wananchi wake ni watu wa kufanyia 'tumbo na mfuko' yaani wanalima kwa ajili ya kupata fedha kidogo ya kuweka mfukoni, lakini hawaangalii namna ya kupiga hatua kimaendeleo.
Akihutubia mamia ya wananchi na viongozi mbalimbali wilayani Chato mkoani Geita jana, wakati akikabidhi shule ya msingi iliyopewa jina lake, Museveni alieleza historia yake na Tanzania ikiwamo kilichomsukuma kurudisha shukrani.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, wakati wa vita ya Tanzania na Uganda chini ya utawala Iddi Amini, (Museveni) aliishi katika kijiji cha Nyamiaga kilichopo mpakani mwa Tanzania na Uganda, katika nyumba ya nyasi na kwamba baada ya kufanikiwa kuchukua nchi na kuwa Rais wa Uganda, alimuomba hayati Benjamin Mkapa atoe msaada kwa kujenga shule eneo hilo.
Alisema katika kipindi chote cha mapigano ya kumuondoa Amini aliishi hapo na kwamba aliamua kujenga shule hiyo, ili iwe zawadi kwa wanakijiji hicho lakini pia kama kumbukumbu.
Aidha, alisema shule nyingine ameijenga katika kijiji cha Muhutwe wilayani Muleba,ambayo alieleza kuwa ilitokana na kuishi katika nyumba moja ya mzee Zakaria Masoud mwaka 1978, wakati wa vita ya Uganda.
Alisema alipokuja Tanzania katika ziara yake pia alimuomba hayati Mkapa ajenge shule katika kijiji hicho cha Muhutwe na hivyo kuitwa Shule ya Msingi Muhutwe.
"Nilipokuja ziara nilienda kumuona Mzee Zakaria Masoud na nikamkuta na familia yake, niliamua kutoa zawadi kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuwajengea Shule ya Msingi,'' alisema Museveni.
Alisema shule ya tatu aliamua kuijenga Chato baada ya hayati Dk. John Magufuli kumkubalia afanye hivyo na kwamba yeye alikubaliana naye, ingawa alisisitiza kwamba hakumuomba kufanya ujenzi huo.
''Hii ni mara ya kwanza kitu kama hiki kuitwa jina langu na hata duniani hakuna kitu cha kijamii kinaitwa jina langu, hata kule kwangu Uganda sitaki kuitwa jina langu vitu vya kijamii,"alibainisha Rais Museveni.
Aliongeza kuwa kitu pekee kilichomfanya kujenga shule hizo ni undugu alionao na Tanzania pamoja na kuweka kumbukumbu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kuhusu wananchi wake kuwa wavivu kwenye kilimo licha ya kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, Rais Museveni alisema hatua hiyo inawakwamisha kufikia maendeleo.
Kwa mujibu wa Rais Museveni, Waganda wengi wanalima kwa ajili ya tumbo, kwa maana ya kupata chakula pamoja na kupata fedha kidogo za kuweka mfukoni.
Aliongeza kuwa kati ya kaya 2,500 moja pekee ndiyo inayofunga walau nguruwe kwa ajili ya kuongeza kipato, lakini waliobaki hawajishughulishi na kazi nyingine.
"Kwa namna hii nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo kwa watu kufanyia tumbo na mfuko na kushindwa kufanya kazi nyingine,'' alibainisha.
SAMIA AMSHUKURU
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika makabidhiano hayo ya shule hiyo, alimshukuru Rais Museveni kwa kuwekeza kwenye elimu.
Alisema shule hiyo itakayokuwa na mitaala ya Kiingereza yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 630, imegharimu dola za Marekani milioni 1.6.
Rais Samia alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo.
Akizungumzia suala la wanafunzi wa shule za sekondari kuruhusiwa kuendelea na masomo wanapopata ujauzito, alisema suala hilo lisichukue muda mwingi kujadiliwa kwa kuwa limeishapitishwa na serikali.
Alisema mwanafunzi wa shule ya msingi akipata ujauzito hataendelea na masomo katika mfumo wa kawaida badala yake atafundishwa njia nyingine ya ujasiriamali na kujiajiri, lakini wale wa sekondari wao wataruhusiwa kuendelea na masomo.
Alisisitiza kuwa wanafunzi wote walioacha shule kutokana na utoro na mimba warudi shule na kuendelea na masomo na wale walioshindwa mitihani ya darasa la saba wapewe nafasi ya kurudia shule.
Akizungumza katika sherehe hizo za makabidhiano, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde, alisema serikali imeongeza bajeti ya elimu bure kutoka Sh. bilioni 21 kwa mwezi hadi kufikia Sh. bilioni 26 kwa mwezi.
Aidha, aliagiza kila kiongozi kuhakikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa fedha za Uviko-19 unakamilika kabla ya Desemba 15, mwaka huu, ili kuwezesha wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kuanza masomo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Prof. Joyce Ndalichako, alisema wanafunzi 9 07, 802 waliomaliza darasa la saba mwaka huu wamepangiwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Alisisitiza kwamba wanafunzi walioacha masomo warudi shuleni na serikali itawapa nafasi nyingine ili kurudia masomo na wakifaulu wataendelea kusoma katika mfumo rasmi wa serikali.