Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatma kesi ya mwanahabari Kabendera 'kutekwa' kujulikana leo

Kabendera As Hatma kesi ya mwanahabari Kabendera 'kutekwa' kujulikana leo

Tue, 10 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne, Septemba 10, 2024 inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la awali lililowekwa na kampuni ya huduma za mawasiliano kwa simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Public Limited katika kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Mwanahabari, Erick Kabendera.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo ya pingamizi la awali lililowekwa na Vodacom ikiiomba Mahakama hiyo isiisikilize, badala yake iifute.

Kabendera alitiwa mbaroni na askari polisi nyumbani kwake Julai 29, 2019 na kushikiliwa kwa siku kadhaa, kisha akafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Kesi hiyo ilimalizika kwa utaratibu wa majadiliano na makubaliano ya kukiri makosa baina yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) unaojulikana kisheria kama plea bargaining.

Aliachiliwa huru Februari 24, 2020 baada ya kulipa fidia na faini aliyoamuriwa na Mahakama baada ya kumtia hatiani kwa kukiri makosa yake kulingana na majadiliano na makubaliano hayo na DPP.

Miaka minne baada ya kesi yake hiyo kumalizika, Kabendera ameifungulia kesi Vodacom akiituhumu kufanikishwa kukamatwa kwake na askari polisi, tukio analoliita kutekwa, kisha kufunguliwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Katika kesi hiyo ya madai namba 12799/2024, Kabendera anayewakilishwa na Wakili Peter Madeleka anadai kutokana na tukio hilo amepata madhara mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live