Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hali ya hewa yakwamisha kazi ya uokoaji wanaohofiwa kufa maji Ziwa Victoria

Ziwa Uokoajiiiii Victoriaaaa.png Hali ya hewa yakwamisha kazi ya uokoaji wanaohofiwa kufa maji Ziwa Victoria

Tue, 17 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kazi ya kutafuta miili ya watu watano wanaohofiwa kufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama Ziwa Victoria imesitishwa kwa muda kutokana na hali mbaya ya ziwa na waokoaji kumeshindwa kuona ndani ya maji.

Watu hao walipata ajali hiyo jana usiku, Septemba 15, 2024, walipokuwa wakirejea eneo la Bulomba, Kijiji cha Igundu kutoka katika kijiji cha Mwiruruma walikokwenda kusherehekea harusi upande wa bibi harusi. Ajali hiyo ilitokea umbali wa kilomita moja na nusu kabla ya kufika Igundu.

Baada ya sherehe kumalizika, upande wa bibi harusi na ndugu wa bwana harusi walipanda mtumbwi kurudi nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya shughuli ya siku ya pili.

Akizungumza eneo la tukio leo Jumatatu Septemba 16, 2024, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kazi ya uokoaji ilianza alfajiri ya leo, lakini zilishindikana kutokana na ukungu na tope jingi lililokuwa ndani ya maji.

Waokoaji saba kutoka Mwanza wakiwa na vifaa zaidi wanatarajiwa kufika kusaidiana na wenzao kutoka Mara.

“Tayari mwili wa Hadija Maregesi (20) umeopolewa. Wengine wanaohofiwa kufariki ni Machumu Machumu (32), Maregesi Robert (30), Nyanjiga Lazaro (39), Mashauri Richard (25) na mmoja ambaye jina lake halijafahamika. Mtumbwi huo ulikuwa na watu 20, watu 14 wameokolewa wakiwa hai,” amesema Magere.

Magere amesema tayari askari saba wa uokoaji na zimamato kutoka Mwanza wakiwa na vifaa zaidi wako njiani kuelekea eneo la tukio kuungana na wenzao wanane wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya utafutaji wa miili hiyo.

"Kuna tope jingi tena jeusi, lakini pia tumekutana na ukungu hivyo tumeshindwa kuendelea na utafutaji wa miili hiyo, tumesistisha kwa muda tukisuburi vifaa zaidi ambavyo vitafika hapa muda wowote," amesema kaimu kamanda huyo.

Amemtaja mtu mmoja ambaye mwili wake uliopolewa tangu jana ukiwa umenasa kwenye nyavu za nanga ya mtumbwi kuwa ni Hadija Maregesi (20).

"Chanzo cha ajali hii inasadikiwa kuwa uzito uliopitiliza, kwani mtumbwi una uwezo wa kubeba watu si zaidi ya watano, lakini kama mnavyoona kulikuwa na watu 20," amesema.

Wakieleza jinsi ajali ilivyotokea, manusura wa ajali hiyo wamesema ilitokea baada ya mtumbwi waliokuwa wamepanda kupasuka na kuanza kujaa maji.

Dabes Msilikale, amesema mtumbwi huo ulipasuka baada ya kupigwa na wimbi na watu waliokuwepo kuanza kuchota maji kwa kutumia makopo na mikono yao.

"Wote tuliokuwa kwenye mtumbwi ni ndugu na jamaa. Mmoja ambaye hajapatikana ni mama mlezi wa bwana harusi. Tulipoona maji yanaanza kujaa, tulijaribu kupiga simu kuomba msaada, lakini hatukupata mawasiliano," amesema Msilikale.

Amesema i walipokuwa wakihangaika kuchota maji, wimbi jingine kubwa liliupiga mtumbwi, kisha ukageuka na kuwazamisha wote ndani ya ziwa. Wakati wakiendelea kupambana na maji, wimbi jingine lilipiga na kuugeuza mtumbwi mara ya pili.

"Tulijaribu kuogelea ili kupanda kwenye mtumbwi, lakini wengine hawakufanikiwa na wengine tuliweza kujiokoa,” amesemaMsilikale.

Amesema baada ya tukio hilo, bwana harusi ambaye aliwahi kufika kwa mtumbwi mwingine alipata mshtuko na kupoteza fahamu, hivyo alikimbizwa hospitali na amelazwa mpaka sasa.

Kutokana na ajali hiyo, harusi iliyokuwa imepangwa imeahirishwa na juhudi zinaelekezwa kwenye kutafuta miili ya ndugu na jamaa waliopotea.

Mbunge wa Mwibara, Charles Kajege amesema tukio hilo ambalo ni la pili kutokea ndani ya miezi 14, ni la kusikitisha hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kuepuka ajali kama hizo.

"Pamoja na yote, wananchi tunatakiwa kuchukua tahadhari, kwani vyombo vilivyotumika si sahihi kusafirisha abiria," amesema.

Amewataka wakazi wa kijiji hicho cha Igundu kuwa na subira, wakati Serikali ikitafuta miili hiyo huku akiwahakikishia kuwa miili yote itaopolewa.

"Niko na nyie hadi tuhakikishe wapendwa wetu wanapatikana na tayari nimeongea na Waziri Mkuu, lakini pia tangu asubuhi mkuu wetu wa wilaya alikuwa hapa na watu wa zimamoto, hii yote ni kuhakikisha miili inapatikana. Pia nitagharamia chakula kwa waombolezaji wote tulioko hapa hadi siku mwili wa mwisho utakapopatikana," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano ameagiza kukamatwa kwa wamiliki wa mitumbwi yote miwili iliyotumika, huku mmoja wao akiwa tayari amekamatwa na mwingine bado anatafutwa.

"Tulishazuia mitumbwi hii ya uvuvi kutumika kusafirisha watu, lakini agizo hili limepuuzwa, naagiza wakamatwe, ili hatua zichukuliwe," amesema mkuu huyo wa wilaya.

Ofisa Tarafa wa Nansimo, Moses Ng'omnaitanga amesema kutokana na agizo hilo la mkuu wa wilaya, tayari mmiliki mmoja amekamatwa, huku mwingine akitafutwa baada ya kutoroka.

Amemtaja anayeshikiliwa kuwa ni Andrea Msimu, mmiliki wa mtumbwi wa kwanza ambao ulifika salama na anayetafutwa kuwa ni Lazaro Msimu.

"Huyu ambaye mtumbwi wake ulisababisha maafa alitoroka baada ya tukio kutokea na alitoroka na mtumbwi wake" amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumera Nyamkinda, ameomba Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wamiliki wa mitumbwi wanaobeba abiria kinyume cha sheria, huku akitaka Serikali kuweka usafiri wa uhakika kwa wakazi wa vijiji vinavyotegemea usafiri wa majini.

Julai 30, 2023 watoto 14 wakiwemo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba iliyopo Kijiji cha Igundu, walifariki dunia baada ya mitumbwi miwili waliyokuwa wamepanda wakitoka kwenye ibada katika Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) kuzama ndani ya Ziwa Victoria, eneo la kijiji cha Mchigondo.

Katika tukio hilo la mwaka jana, watu 14 waliokolewa wakiwa hai, huku chanzo cha tukio likielezwa kuwa ni mitumbwi hiyo kuzidisha uzito.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live