Waziri wa Nishati, January Makamba amesema miradi sita ya umeme katika Kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme kwenda Mkoani Kigoma na Geita iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 600 hadi kukamilika kwake.
Makamba ameyasema hayo hii leo Oktoba 16, 2022 wakati akitoa taarifa mbele ya Rais Samia, ambaye alizindua miradi hiyo kwenye hafla iliyofanyika Nyakanazi Mkoani Kagera, nakuongeza kuwa miradi mingine iliyobaki itachukua muda mrefu kukamilika, kutokana na uhitaji wa utaalamu wa hali ya juu.
Amesema, kituo hicho Kinahudumia wilaya za biharamulo na Ngara na pia kinapeleka umeme mkoa wa kigoma katika Wilaya za Kakonko, Kasulu na Kibondo na kwamba pia kimetumika kupeleka gridi ya taifa katika Mkoa wa Kigoma kwa mara ya kwanza.
Aidha, Waziri Makamba amefafanua kuwa kituo hicho kitaboresha huduma ya umeme wa uhakika katika Wilaya ya Ngara na kuondosha shida za awali za kama kupampu maji na matumizi ya Jenereta na kwamba kitapoza umeme kutoka kilovoti 220 had 33 kilovoti.
Kwa upande wao, Mbunge wa jimbo la Biharamulo, Mhandisi Ezra Chiwelesa na Mbunge wa Ngara, Ndaisaba George Ruholo wamemshukuru Rais Samia kwa kuboresha sekta ya nishati inayokwenda kumaliza tatizo la umeme, hasa kwa wafanyabiashara na wawekezaji waliokuwa wakikosa uhakika wa umeme.
Awali, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila alisema kupatikana kwa kituo hicho cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme Nyakanazi, kitasaidia uzalishaji wa uhakika katika migodi ya Stamigold na Kabanga Nikel ambayo imekuwa ikitumia fedha nyingi kununulia mafuta ya kuendesha mitambo.